Wachezaji wa timu ya Madiwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Kocha wao Bakari Ngoda (hayupo pichani) wakati wa mapumziko. |
Jioni ya leo katika Wilaya ya Mkalama imewekwa historia
baada ya kuchezwa mchezo wa mpira wa Miguu kati ya timu ya Madiwani wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na timu ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya
ya Iramba huku kikosi cha timu ya Iramba kikiongozwa na Waziri wa mambo ya
ndani Mhe. Mwigulu Nchemba.
Katika Mchezo huo uliomalizika kwa timu ya Madiwani wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kufungwa jumla ya magoli 3-1 kulikuwa na
vivutio mbalimbali huku burudani kubwa ikiwa ni kiwango kizuri kilichokuwa
kikioneshwa na Mhe. Nchemba na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
Mhandisi Godfrey Sanga ambaye ndiye alikuwa mfungaji wa bao pekee la timu ya
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ilianza kuhesabu kalamu
yake ya magoli kupitia kwa Mshambuliaji wake tishio katika mcheo wa leo Mhe.
Mwigulu Nchemba ambaye alifunga goli hilo baada ya kuachia shuti kali kufuatia
mpira uliompita beki wa timu ya Mkalama John Tibu.
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya kuelekea
mapumziko, Kiungo wa timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey
Sanga aliisawazishia timu yake goli baada ya kukwamisha kiufundi wavuni penati
yake iliyotokana na beki wa timu ya Iramba kuunawa mpira wakati akiwa kwenye
heka heka za kuokoa mpira uliopigwa na Mshambuliaji Lunzegere Kilala.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu
hizo zilikuwa zimetoshana nguvu baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Maelekezo ya walimu wa timu zote mbili wakati wa mapumziko
yalionekana kuzaa matunda zaidi upande wa timu ya Iramba baada ya kufanikiwa
kupachika goli la pili kupitia kwa Mhe. Mwigulu Nchemba kwa mara nyingine tena
huku safari hii akifunga goli hilo baada ya “piga nikupige” zilizotokea katika
goli la timu ya Mkalama.
Mara baada ya kufungwa goli la 3 lililofungwa dakika 10 tu
baada ya goli la pili, timu ya Mkalama ilifanya mabadiliko ya wachezaji hatua
ambayo yalionesha mafanikio baada ya timu hiyo kuongeza kasi ya mashambulizi
lakini hata hivyo kasi hiyo haikuweza kuzaa matunda kutokana na uhodari
uliooneshwa na kipa wa timu ya Iramba ambaye alipangua michomo kadhaa iliyokuwa
ikielekezwa golini kwake.
Mara baada ya kumalizika kwa Mchezo, Nyota wa mchezo huo
ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Iramba
Magharibi Mhe. Mwigulu Nchemba aliushukuru Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama kwa maandalizi mazuri ya tukio hilo huku akiomba jambo hilo liwe
endelevu.
“Mimi na Mhe. Kiula tukiwa bungeni huwa tunashughulikia
changamoto zetu kwa pamoja kwa sababu kwetu Iramba ni moja hivyo ni vizuri ushirikiano
huu tuuenzi na kuudumisha” Aliongeza Mhe. Nchemba.
Akijibu ombi fupi lililowasilishwa na Mbunge wa jimbo la
Mkalama Mhe. Allan Kiula kuhusu umaliziwaji wa kituo cha polisi kilichopo
Nduguti, Mhe. Nchemba alisema kuwa katika bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani
inayotarajiwa kusomwa tarehe 30 mwezi
huu, kipaumbele cha Ujenzi na uboreshaji wa vituo vya polisi kimewekwa Wilaya mpya zote ikiwemo Wilaya ya
Mkalama.
“Lakini pia ombi la Mhe. Kiula la kutaka timu ya madiwani
wa Halmashauri zote mbili za Iramba na Mkalama kucheza na timu ya bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepita hivyo tutakaa na Mhe. Kiula na kupanga
tarehe rasmi ya mechi hiyo” Alisisitiza Mhe. Nchemba.
Mchezo huo ulitanguliwa na Mkutano wa baraza la madiwani
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama robo ya pili uliofanyika mapema asubuhi
ambapo kamati mbalimbali ziliwasilisha taarifa zao na waheshimiwa madiwani
kupata nafasi ya kuuliza maswali ya papo kwa hapo kwa Wenyeviti wa kamati hizo,
Mkurugenzi na Wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
No comments:
Post a Comment