Thursday, 26 April 2018

Muungano huu ni wa kuuenzi-MASAKA

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandsi Jackson Masaka akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika kijiji cha Iguguno leo.

Kikundi cha Ngoma za asili kutoka katika kijiji cha iguguno kikitumbuiza kwenye maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika kijiji cha Iguguno leo.

PICHA MBILI CHINISehemu ya wananchi walijitokeza kwenye maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika kijiji cha Iguguno leo.

“Kama umeshindwa kumsikiliza mama yako mzazi aliyekuzaa, utanisikiliza mimi Mkuu wa Wilaya?”

Hilo ni swali alilouliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo katika ngazi ya Wilaya yamefanyika katika kijiji cha Iguguno.

Mhe. Masaka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo aliuliza swali hilo wakati akiwasisitiza wananchi wa Wilaya ya Mkalama kujenga utamaduni wa kumaliza matatizo yao wenyewe badala ya kusubiri viongozi wa serikali waingilie kwenye matatizo hayo.

“Ni aibu kwa watu wa familia moja kutegemea watendaji wa serikali kumaliza migogoro yao hivyo ni lazima kila mwananchi kwa nafasi yake ahakikishe anashiriki kikamilifu katika kutatua migogoro inayomkabili ndani ya familia yake” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka aliongeza kuwa kama matatizo hayo yataonekana kuzidi uwezo wa familia husika, ni vizuri hatua stahili za kushughulikia matatizo hayo zikafuatwa kwa kuanza kuyafikisha serikali ya kijiji, kata na tarafa kabla hayajafika katika ofisi yake.

Akitoa ujumbe wa maadhimisho ya Muungano ya Mwaka huu Mhe. Masaka amewataka wananchi kuhakikisha wanadumisha na kuuenzi Muungano huo huku akiwataka  kupuuza  kauli za baadhi ya watu wachache wanaobeza faida kubwa zinazopatikana ndani ya pande zote mbili za Muungano huo.

“Wewe Mwananchi wa Lukomo au Nyeri, una mashamba yako na umepata mazao ya kutosha, inakusaidia nini kuhoji kwanini Rais wa Zanzibar naye anapanda ndege?” Aliuliza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka aliwasihi wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuhakikisha wanalinda na kuitunza amani na utulivu uliopo hivi sasa huku akikisisitiza kuwa serikali haitafumbia macho aina yoyote ya viashiria vya uvunjifu wa amani vitakavyoonekana na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaoonesha viashiria hivyo.

Kuhusu kampeni ya kitaifa ya chanjo ya kujikinga na saratani ya Mlango wa kizazi inayoendelea hivi sasa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 Mhe. Masaka amewataka wazazi wote kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo katika vituo vitakavyotajwa ili kuwaepusha wasichana hao na tatizo hilo ambalo linazidi kuwa kubwa kila Mwaka.

“Kila Mwaka saratani ya mlango wa kizazi husababisha vifo vya wanawake zaidi ya 2000 nchi nzima hivyo asitokee mzazi yoyote kumkataza mwanae kupata chanjo hiyo kisa yeye hakuwahi kupatiwa kwa sababu miaka inabadilika na tatizo hili linazidi kuwa kubwa ndio maana Serikali imeamua kuchukua hatua” Alisisitiza Mhe. Masaka.


Mhe. Masaka alimalizia hotuba yake kwa kuwasihi wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli ambapo pia aliwataka waendelee kumuombea afya njema ili aendeleze jitihada za kuhakikisha Tanzania Mpya inasonga mbele.

Tafadhali Bonyeza hapa ili uweze kumuona Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati akihutubia leo.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA