Saturday, 28 April 2018

MKALAMA YASHEREHEKEA SIKU YA MKULIMA

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia leo katika sherehe za Siku ya Mkulima zilizofanyika katika kijiji cha Kidarafa.

Mwakilishi wa Kampuni ya Usambazaji wa mbolea inayojulikana kifupi kama "ETG" ndugu Cosmas Maganga akitoa maelekezo juu ya namna ya kutumia  moja ya dawa za kuua wadudu shambani wakati wa sherehe za siku ya Mkulima zilizofanyika leo katika kijiji cha Kidarafa.

Mkurugenzi wa Kampuni inayojulikana kama "Meru Agro tours" Bi. Cecilia Magesa akitoa maelezo ya njia za kupata mazao ya kutosha kwa Mkulima wakati wa sherehe za siku ya Mkulima zilizofanyika leo katika kijiji cha Kidarafa.Wilaya ya Mkalama leo imefanya sherehe za siku ya Mkulima iliyofanyika katika kijiji cha Kidarafa kwa kuwajengea uwezo wakulima kutambua umuhimu wa kutumia pembejeo bora na za kisasa.

Sherehe hizo zilizofanyika kwa mtindo wa Warsha fupi kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbegu na mbolea iliwezeshwa na wasambazaji maarufu wa pembejeo za kilimo wanaojulikana kama “BAYDA AGROVET”  wakishirikiana na Kampuni ya kizalendo ya uuzaji wa mbegu bora na za kisasa, viautilifu na madawa mbalimbali ya mimea inayojulikana kama “Meru Agro tours” yenye makao yake makuu Mkoani Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizo,  alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuwasisitiza wakulima kutumia vyema elimu waliyopewa  katika warsha hiyo kuhakikisha wanafanya kilimo bora na cha kisasa.

Mbali na msisitizo huo, Mhe. Masaka pia alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wakulima wote Wilayani hapa wahakikishe wanapata pembejeo kwenye maduka rasmi na waombe risiti ya kuthibitisha manunuzi yao.

“Epukeni kununua pembejeo kwenye minada au maduka yasiyo rasmi kwa sababu tutashindwa kumpata muuzaji pindi ikigundulika kuwa bidhaa uliyonunua ni feki” Alisisitiza Mhe. Masaka.

Mpaka sasa kampuni ya “Meru Agro tours”  imefanikiwa  kutoa elimu kwa wakulima kutoka katika kata tano za Mwanga, Nduguti,Ilunda, Nkalankala na Kinampundu.

Mafunzo hayo ambayo yalijumuisha wakulima mmoja mmoja 42 na vikundi 25 vyenye jumla ya wakulima 625 yalienda sambamba na ugawaji wa kilo 133 za mbegu bora za mahindi zenye thamani ya shilingi 798,000, kilo 300 za mbolea aina ya DAP, kilo 300 za mbolea aina ya Urea na kilo 50 za mbolea aina ya Kyno vyote vikigharimu shilingi 648,000 na hivyo kufanya jumla ya mchango uliotolewa na kampuni hiyo Wilayani Mkalama  mpaka sasa kufikia kiasi cha shilingi milioni 1,446,000.

Siku ya Mkulima Wilayani Mkalama huadhimishwa kila mwaka muda mfupi kabla ya kuanza kwa msimu wa mavuno ya mazao mbalimbali.
No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA