Monday 30 April 2018

Chanjo zinaokoa gharama za matibabu-Masaka

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akitoa hotuba katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi.

Diwani wa kata ya Nduguti Mhe. Loth Dia akizungumza katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi.

Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto  (DRCHCO) Wilayani Mkalama Daniel Basso akisoma taarifa fupi kuhusu saratani ya Mlango wa kizazi katika uzinduzi wa chanjo ya saratani hiyo uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi. 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ndugu Abdallah Njelu akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi.  

Mganga wa Zahanati ya Nduguti, Dokta Lazaro Chambo akitoa chanjo kwa mmoja wa wanafunzi waliofika katika uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akikabidhi dawa ya chanjo ya saratani ya Mlango wa kizazi kama ishara ya uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika katika zahanati ya Nduguti leo asubuhi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (kushoto walioketi) akiwa na Diwani wa Kata ya Nduguti Mhe. Loth Dia (katikati), Katibu wa Umoja wa wanawake Wilaya Fatuma Ndee na wataalam wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Nduguti.



“Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye Afya, Timiza wajibu wako” Ni kauli mbiu iliyobeba kampeni ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa Miaka 14 iliyozinduliwa rasmi leo Wilayani Mkalama.

Uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa dini na jamii, wanafunzi wa sekondari na wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka.

Katika uzinduzi huo Mhe. Masaka aliwasisitiza wananchi kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 ili wakapate kinga ya saratani hiyo ambayo kila mwaka husababisha vifo vya wanawake 4216 hapa nchini.

“hii ina maana kila siku wastani wa wanawake 11 hufariki dunia hapa nchini kutokana na saratani hii takwimu ambayo ni kubwa sana hivyo wananchi tuhakikishe tunawapa mabinti zetu chanjo hii ili kushusha na kutokomeza kabisa  ugonjwa huu kwa akinamama” Aliongeza Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka alisisitiza kuwa wananchi wakipata chanjo itawapunguzia gharama za matibabu kwa sababu suala hilo hivi sasa limekuwa mzigo mkubwa sana kwa mwananchi wa kawaida.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Loth Dia aliwataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama kuondoa dhana potofu kuwa chanjo huongeza zaidi maradhi na kuwataka kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea chanjo hiyo.

“Siku za nyuma wanawake wengi walipoteza maisha kwa sababu hakukuwa na chanjo ya Ugonjwa huu hivyo tunaishukuru serikali kwa kuokoa maisha ya kizazi kilichopo kutokana na ugonjwa huu wa saratani ya Mlango wa kizazi na wananchi tuiunge Mkono kwa kuhakikisha watoto wetu wanajitokeza kwa wingi kwenda kupatiwa chanjo hii” Alisema Mhe. Dia.

Kwa mwaka 2018 Wilaya ya Mkalama imelenga kutoa chanjo kwa wasichana 2783 ambao walizaliwa mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA