Tuesday 8 May 2018

Mkalama yatengewa fedha za hospitali ya Wilaya

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akizungumza kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti ili aweze kufungua baraza la madiwani lililofanyika leo.

Baadhi ya madiwani wakipitia nyaraka mbalimbali wakati wa baraza la madiwani lililofanyika leo.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Loth Dia akisoma taarifa ya kamati yake ya Fedha, Mipango na Utawala wakati wa baraza la madiwani lililofanyika mapema leo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James  Mkwega  akizungumza machache muda mfupi kabla ya kufunga baraza la madiwani lililofanyika leo.

Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi na Mazingira Mhe. Mohamed Juma akisoma taarifa fupi ya kamati yake wakati wa baraza la madiwani lililofanyika leo.


Baada ya jitihada za muda mrefu zilizofanywa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, hatimaye serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kupitia bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2018/2019  imeidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya.

Habari hiyo njema imetolewa na kuthibitishwa na Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula wakati wa kikao cha baraza la robo ya pili la madiwani lililofanyika mapema  leo katika Ofisi ya Halmashauri hiyo.

“Upatikanaji wa hospitali itakuwa ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Mkalama ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma muhimu na za msingi  za matibabu” Alisema Mhe. Kiula.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga amesema hospitali hiyo itajengwa kwa mtindo wa ghorofa na tayari eneo itakapojengwa hospitali hiyo limeshatengwa na miundombinu ya barabara kuelekea kwenye hospitali hiyo tayari imeshawekwa.

Akizungumzia jambo hilo kabla ya kufunga baraza la leo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega amempongeza mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula kwa ushirikiano mkubwa alioutoa katika kipindi chote cha ufuatiliaji wa kuhakikisha fedha hizo zinatengwa.

“Pia ingawa wanasema beki hasifiwi, nitumie fursa hii kukupongeza sana Mkurugenzi Mtendaji kwa utendaji wako mzuri uliosaidia jambo hili kufanyika kwa sababu pamoja na sifa nzuri zinazokuja kwetu wanasiasa bado ukweli unabaki kuwa nyie watendaji ndio wafanikishaji wa haya mambo kwa kiasi kikubwa sana” Alimalizia Mhe. Mkwega.


Uidhinishwaji wa fedha za ujenzi wa hospitali ya Wilaya inakuwa ni muendelezo wa habari njema katika sekta ya Afya Wilayani Mkalama  baada ya siku kadhaa zilizopita kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 na serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni 400 za Uboreshaji wa kituo cha Afya cha Kinyambuli ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika.




MASWALI NA MAJIBU YA BARAZA LA MADIWANI LILILOFANYIKA LEO MEI 08, 2018.

Swali la 1.    Mhe. Amri Gyunda (kata ya Msingi): Ni lini Mbwa wanaozurula mitaani Wilayani Mkalama watawekewa utaratibu mzuri ili wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi?

Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Mbwa wote wanapaswa kuwekwa katika mazingira mazuri na kufungwa na wamiliki wao lakini kutokana na hoja yako Mhe. Amri, tutaanza kuwachukulia hatua wamiliki wote wanaoacha mbwa wao wazurule ovyo mitaani.

Swali la 2. Mhe. Eunick Kalaila (Viti maalum Kinyangiri): Ni lini huduma ya baraza la ardhi la Wilaya itaanza kutolewa Wilayani Mkalama?

Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Taratibu zimefanyika na wahusika walifika hapa Wilayani kwa ajili ya kukagua jengo lililopendekezwa kufanyia baraza hilo hivyo tunachosubiri hivi sasa ni mrejesho wa ukaguzi wao kama wameridhika na jengo hilo au la.

Swali la 3. Mhe. Bilal Msengi (kata ya Tumuli):  Ni lini jina la jimbo la Iramba Mashariki litabadilishwa na kuitwa jimbo la Mkalama?

Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Suala la kubadilisha majina ya majimbo lipo chini ya Tume ya Uchaguzi lakini tayari tulishawaandikia na tunachosubiri hivi sasa ni majibu kutoka kwao.

Jibu la Nyongeza- Mhe. James Mkwega (Mwenyekiti wa Hw)- Waheshimiwa madiwani mimi nadhani jina Iramba Mashariki lingebaki kuwa hivyo kwa sababu tukibadilisha jina tutapoteza asili yetu na ikumbukwe jina hili linamaanisha sisi ni watu wa Iramba.

Swali la Nyongeza. Mhe. Bilal Msengi (kata ya Tumuli: Kuna mpango gani wa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya watu jamii ya wahadzabe ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo?

Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Ni kweli jamii ya wahadzabe ni watu maalum sana na ni moja ya alama inayotutangaza vizuri nje ya hapa lakini kutokana na mpango wa kukabiliana na uharibifu wa Mazingira, mipango inafanyika ili kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya wahadzabe kufanya shughuli zao.

Jibu la Nyongeza- Mhe. Allan Kiula (MB)- Madiwani wote tunapaswa kuwa wasimamizi wa matumizi bora ya ardhi na maeneo hivyo ni wajibu wetukukaa na kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kila kata inakuwa na mpango wa matumizi bora ya Ardhi.

Swali la 4. Mhe. Omary Nzia (kata ya Miganga): Ni kwa nini Maafisa watendaji wa wa vijiji wanalipwa nusu ya malipo wanayostahili wakati wa kustaafu?

Jibu: Khashim Lugome (Afisa Utumishi) – Hakuna afisa Mtendaji anayelipwa nusu ya mafao yake kwa sababu wote wanalipwa kutokana na mchango waliochangia na pia wamekidhi vigezo vya msingi kwa kuchangia miezi 180 ya utumishi mfululizo.

Kama mtumishi yoyote aliajiriwa na Halmashauri na kulipwa mshahara wake wote na Halmashauri bila kukatwa makato yoyote kisha akaajiriwa na kwa mkataba wa kudumu na serikali ni wazi hatopata mafao ya kipindi alichokuwa na mkataba wa muda kwa sababu hakuwa akikatwa.

Swali la 5. Mhe. Abiba Omary (kata ya Kinampundu viti maalum): Eneo lililotengwa hapo awali kwa ajili ya matumizi ya kujenga uwanja wa mpira wa miguu limebadilishwa matumizi na kuwa eneo la Soko, je lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya Uwanja?

Jibu: Mhandisi Godfrey Sanga (DED)- Ndio lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu katika kijiji cha Maziliga.


1 comment:

  1. Binafsi sioni sababu ya jina la iramba mshariki kubadilishwa Ni jina lenye utambulisho mzuri...pia Ni nembo yetu sisi wanyiramba wote.
    Pia ni vema mkurugenzi,ashirikiane vema na tanesco au REA ili kufikisha umeme katika vijiji na kuhimiza kila kaya kujinga na matumiz ya nishati hiyo.

    ReplyDelete

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA