Wednesday, 13 December 2017

Serikali hii haitaki ubabaishaji- Nyongo

Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo  (Wapili kutoka kulia) akielekea kwenye kinu cha kuchenjulia Madini katika Mgodi wa Tumuli mapema leo.

Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo juu ya namna kazi inavyofanyika katika Mgodi wa Tumuli Mapema leo.

Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika kata ya Tumuli mapema leo.

Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Tumuli (Hawapo pichani) alipofanya Ziara katika Wilaya ya Mkalama mapema leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akitambulisha Wataalam alioambatana nao wakati wa Ziara ys Naibu Waziri wa Mdini Mhe. Stanslaus Nyongo.

Mwenyekiti wa Hlmashauri ya Wilaya ya Mkalama akitoa neno la Shukrani kwa Naibu Waziri wa MadiniMhe. Stanslaus Nyongo alipomaliza kuzungumza na Waachimbaji wadogo.Katika muendelezo wa ziara za viongozi wakuu mbalimbali wa serikali ya Awamu ya Tano Wilayani Mkalama leo ilikuwa ni zamu ya Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye alifika katika kata ya Tumuli kwa ajili ya kusikiliza na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Mgodi wa madini ya dhahabu uliopo kwenye kata hiyo ambao unaohusisha Wachimbaji wadogo na mwekezaji mwenye uraia wa China.

Mara baada ya kufika Shule ya Msingi Tumuli ambako ndipo alipofanyia Mkutano baina yake na Wachimbaji hao wadogo Mhe. Nyongo aliwataka viongozi wa Chama cha Wachimbaji hao kumueleza kwa kina mchakato mzima wa suala hilo mpaka kufikia  katika hatua ya Mgogoro.

Akielezea mchakato mzima ulivyokuwa mmoja wa viongozi wa wachimbaji hao Bw. Salum Kapalale alisema kuwa wachimbaji wote wadogo waliopo katika kata hiyo walikuwa wanamiliki jumla ya maduara 90 huku yakitoa fursa ya ajira kwa watu 1243 kabla ya Mzawa mmoja akishirikiana na mwekezaji kufika na kuwaondoa katika maeneo yao.

“Tangu tumeanza uchimbaji wa Madini mnamo mwaka 2007, eneo la Mgodi lilikuwa wazi mpaka ulipofika mwaka 2010 ambapo mtu anayefahamika kwa majina ya Salum Kondo alifika na kudai kuwa yeye ni mmiliki wa eneo lote la uchimbaji ambapo baada ya kuzungumza naye tulikubaliana kushirikiana naye katika shughuli za uchimbaji” Aliongeza Kapalale.

Kwa mujibu wa Kapalale hali ya taharuki iliendelea kutanda mwaka 2012 baada ya mwananchi mmoja aliyetambulika kwa majina ya Ibrahim Sadof Shakama kufika katika eneo hilo la Mgodi na kudai kuwa eneo hilo ni la marehemu baba yake mzazi hivyo aliwataka wachimbaji hao wampe eneo hilo ili ampe mwekezaji Mkubwa  ambaye mbali na kuwalipa fidia wachimbaji hao, pia watapata ajira katika Mgodi huo watasaidia kujenga miundombinu mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo kabla hawajaanza shughuli za uchimbaji wa madini hayo.

Kufuatia makubaliano hayo wachimbaji hao walikubali kumuachia Bw. Shakama eneo hilo huku wakisubiri kutekelezewa makubaliano yao jambo ambalo halikufanyika kabisa na badala yake waliishi bila ajira yoyote kuanzia Mwaka 2012 mpaka Mwezi Juni 2016 ambapo  Mwekezaji mwenye Uraia wa China alifika na  kuanza kazi Mgodini hapo na walipojaribu kumfuata Bw. Shakama kuhusu makubaliano yao ya awali aliwajibu kuwa wao ni wachimbaji wadogo hivyo hawatambuliki.

“Jibu hili lilituvunja moyo sana na ndipo tulipoanza kuchukua hatua mbalimbali za kudai haki yetu ambapo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Sospeter Mhongo alifika hapa na baada ya kusikiliza pande zote alitoa siku 7 kwa Uongozi wa Wilaya kuhakikisha umemalizika ambapo baada ya Mhe. Waziri kuondoka  Mhe. Mkuu wa Wilaya pia alitoa siku 14 kwa mwekezaji huyo kuhakikisha amelipa fidia yote anayodaiwa jambo ambalo halijatekelezwa mpaka leo” Aliongeza Kapalale.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula mbali na kumshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kukubali wito wake na kufika katika eneo hilo, Alimtaka Kamishna wa Madini wa kanda ya kati kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo kwani migogoro mingi ya madini Wilayani hapa  inatokana na ofisi yake kutosimama imara.

“Mhe. Naibu Waziri Namuomba sana Kamishna wa Madini kanda ya kati atusaidie sana katika mambo kama haya kwa sababu ninaamini kama akiivaa taaluma yake ipasavyo hatutafikia katika hatua ya Migogoro ya aina hii ambayo kama wananchi wa Mkalama wangekuwa ni wakorofi basi kungekuwa na maafa makubwa sana hapa” Alisema Mhe. Kiula.

Mhe. Kiula alimalizia kwa kuwapongeza wananchi hao kwa Utulivu Mkubwa walioanao wakati wa migogoro na wawekezaji ambapo aliwahakikishia kuwa atakuwa nao bega kwa bega kwa kuwaletea viongozi husika katika kila jambo linalowaletea vikwazo vikubwa kwenye  Maendeleo yao.

Akizungumza mara baada ya kupata picha kamili ya mgogoro huo, Mhe. Nyongo alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na wajanja wachache wanaojua taratibu na sheria ambao bila kupitia ngazi za viongozi husika wanapitisha baadhi ya mambo ambayo baadae hugeuka kuwa mateso kwa wananchi wa kipato cha chini.

Mhe. Nyongo aliongeza kuwa hata majibu ya dharau ya kiburi yanayotolewa kwa wananchi kutoka kwa wawekezaji hao yanatokana na wawekezaji hao kujua fika kuwa sheria itawalinda pindi wananchi hao watakapowashtaki.

“Sasa mimi nisiseme maneno mengi, ninajua hata nikitoa siku ngapi maagizo yangu hayatotekelezwa hivyo ninasimama na wananchi wangu kudai haki yao na sina haja ya kupoteza Muda, Hivyo Mhe. Kamishna wa Madini fanya mpango Keshokutwa wakati napita hapa  nionane na hao watu watatu ambao ni Ibrahim,  Salum na huyo Mwekezaji nibanane nao ili wanapokuja kwenye kikao cha tar 19 waje na jibu lililonyooka” Aliagiza Mhe. Nyongo.

Mhe. Nyongo Alisisitiza  kwa kutoa onyo kwa watu wote wenye ujanja wa aina hiyo kuacha mara moja kwani serikali hii hairuhusu hata kidogo matumizi ya njia za mkato katika kudhulumu haki za wananchi wanyonge.

“ Kwenye serikali hii ya Mhe. John Magufuli ubabaishaji hauna nafasi hata kidogo hivyo asipowalipa haki zenu tutasimamisha mradi wake” Alimalizia Mhe. Nyongo.No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA