Wednesday, 24 January 2018

Ziara ya Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega (kushoto)  akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kinyangiri Mwalimu Vicent Sholomella wakati wa Ziara ya Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala mapema jana.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibololo Mwalimu Alphonce Michael (kushoto) akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa madarasa na vyoo unaoendelea katika shule hiyo wakati wa Ziara ya kamati ya Fedha, Mipango na Utawala.

Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Mkalama Bi. Rose Kibakaya (katikati) akifafanua jambo wakati wa ziara ya kamati ya Fedha, Mipango na Utawala katika shule ya Msingi Kibololo juzi.

Wajumbe wa kamati ya Fedha, Mipango na Utawala wakikagua jengo la bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Iguguno linaloendelea kujengwa na mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).Kamati ya Fedha, mipango na Utawala kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imefanya ziara yake juzi na jana ambapo ilitembelea miradi mbalimbali ya Maendeleo hususani inayohusu sekta ya Elimu na Maji.

Ziara hiyo ilihusu vijiji vya Nduguti Makao Makuu ya Halmashauri unapoendelea  mradi wa Ujenzi wa Ukumbi bora na wa kisasa wa Mikutano, kijiji cha Ishenga inapopatikana shule ya watoto wenye mahitaji maalum, Kijiji cha Kinyangiri ulipofanyika ujenzi wa Bweni la kisasa la wasichana katika shule ya sekondari ya Kinyangiri, Kitongoji cha Kibololo yanapojengwa madarasa ya kisasa na vyoo vya Shule ya Msingi Kibololo, Kijiji cha Iguguno linapojengwa bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Iguguno, Kijiji cha Senene yanapojengwa madarasa na vyoo vya Kisasa katika shule ya Msingi Senene, Kijiji cha Tumuli yanapojengwa madarasa ya kisasa ya Shule ya Sekondari ya Tumuli,Kijiji cha Kitumbili yanapojengwa madarasa katika shule ya Msingi Kitumbili, Kijiji cha Mgolombyo yanapojengwa madarasa ya Shule shikizi ya Mgolombyo na Kijiji cha Nyahaa unapojengwa mradi wa Maji wa Kijiji hicho.

Katika vijiji vyote ambavyo Kamati imepita pamoja na mambo mengine, wajumbe wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega waliagiza Kamati za Shule zijikite zaidi katika kuinua taaluma badala ya kushughulika na matumizi ya fedha za shule pekee.

Pia kamati ilitoa onyo kwa walimu wote wanaokunywa pombe muda ambao wanapaswa kuwa darasani ambapo iliwaagiza viongozi wa vijiji kuwakamata walimu hao na wale wote wanaokunywa nao na kuwafikisha katika vituo vya polisi ili iwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia kama hiyo.

Mbali na walimu wanaokunywa pombe muda wa kazi, Kamati hiyo pia imepiga marufuku wanafunzi wote katika Wilaya ya Mkalama kutoonekana katika kumbi za starehe, kukesha katika kumbi za televisheni wakiangalia mpira na  kutumia simu za Mkononi wakati wote wakiwa shuleni au nyumbani ambapo Mwanafunzi atakayebainika kupuuza agizo hilo atachukuliwa hatua yeye pamoja na Mzazi wake.

Wakihitimisha ziara yao katika kijiji cha Nyahaa, wajumbe wa kamati walioneshwa kusikitishwa na kasi ya Mkandarasi katika utekelezaji wa mradi wa maji wa kijiji hicho jambo lililolalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu ambapo walitoa agizo kwa Mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo ifikapo Mwisho wa Mwezi huu vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Ziara za kamati mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama hufanyika mara kwa mara huku lengo kuu likiwa ni kufika na kukagua maeneo yote yenye miradi iliyogharamiwa na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA