Saturday 24 May 2014

ZIARA YA KATIBU MKUU WA CCM WILAYANI MKALAMA.

Katibu Mkuu wa CCM - Taifa akiongea na wananchi wa Gumanga
Wananchi wa Mkalama leo walikuwa kwenye shamrashamra za kumpokea Mh. Abrahman Kinana Ambaye ni katibu mkuu wa CCM Taifa aliyefika katika Wilaya ya Mkalama kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM. Akitokea Iramba Mh. Kinana alipokelewa katika wilaya ya Mkalama mnamo saa mbili asubuhi (8:00 am) ambapo mara baada ya kufika alikwenda moja kwa moja kukagua Daraja la Sibiti linalojengwa ambalo litafungua mawasiliano na wilaya ya Meatu.


Wakiwa katika furaha kubwa wananchi wa Mkalama walicheza kwa bidii na katika kuonyesha furaha yao walipiga na kucheza ngoma ya Kinyiramba ijulikanayo kama MBUTU ngoma ambayo hupigwa kwenye matukio maalum. Pia kwaya na vikundi mbalimbali vya filimbi viliwafurahisha watu waliojitokeza kuhudhuria mkutano.
Mwananchi akikatika.

Wananchi wa Mkalama wakipiga
 na kucheza ngoma ya MBUTU

Mzee akipuliza mbutu.

Baada ya hapo alihutubia wananchi wa kijiji cha Gumanga, Nduguti, Nkungi na Iguguno ambapo aliwataka kutokubweteka na watu wanaojidai kutetea maslahi ya nchi kwa kudai serikali tatu na badala yake wamesahau kuwaletea wananchi maendeleo. Pamoja na hayo Mheshimiwa Kinana alivitaja vijiji vitakavyopata umeme ikiwa ni juhudi za CCM kuwaletea maendeleo wananchi, vijiji hivyo ni Kinyangiri, Ishenga, Nduguti, Gumanga, Kisuluiga, Nkalakala, Mwando, Iambi, Ilunda n.k katika kusisitiza jambo hilo aliwataka wananchi kujiandaa kulipia tsh 27,000 ili waingiziwe umeme katika hatua ya awali ambayo ni bei nafuu sana. Pia alivitaja vijiji vya Nkinto, Matongo, Munguli, Dominiki n.k ambavyo vitapata mawasiliano ya simu. Mheshimiwa kinana pia aliwaeleza wananchi wa Nkungi kuwa barabara inayotoka Singida kupitia Ilongero, Mtinko Singa, Nkungi, Mpaka Nduguti ipo kwenye mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha lami na barabara ya Iguguno, Nduguti, Ibaga kupitia daraja la sibiti itakuwa ya lami jambo ambalo litaleta maendeleo kwa wananchi wa Mkalama. Pia zaidi ya Tsh 2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Wilaya, Halmashauri na Nyumba za watumishi.
Nape Nnauye naye alizidi kuwaomba wananchi kuendelea kukiamini chama cha mapinduzi kwa kuwa ndio chama pekee kitakachowaletea maendeleo.
Nape Nnauye

Mh. Mwigulu Nchemba


Mheshimiwa Kinana aliambatana na Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Naibu katibu Mkuu na Mbunge wa Iramba Magharibi, Salome Mwambu Mb. wa jimbo la Iramba Mashariki (Mkalama), Mather Mlata Mbunge Viti Maalum na M/kiti CCM Mkoa Mh. Msindai. Pia Mkuu wa Mkoa wa Singida Kone na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Edward Ole Lenga nao walikuwepo kwenye ziara hii. Pamoja na viongozi wengine mbalimbali walijumuika kumuunga mkono Katibu Mkuu kwenye ziara hii Muhimu.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA