Thursday 13 April 2017

Wakulima wasidhulumiwe-Masaka

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka akitoa maelekezo juu ya ufungashaji sahihi wa vitunguu ambao utamtendea  haki  Mkulima.

Afisa Kilimo na Ushirika  wa Wilaya ya Mkalama  Bw. Cuthbert Mwinuka (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa dereva wa lori aina ya Fuso ambalo lilipakia Vitunguu katika ufungashaji usiokubalika.

Meneja wa Wakala wa  vipimo wa Mkoa wa Singida, Bw. Albogast Kajungu akiwaonesha wakulima na wafanyabiashara mfano wa gunia linalotakiwa kutumika kwa ajili ya kufungashia mazao.

PICHA MBILI CHINI NI JINSI VITUNGUU VILIVYOKUWA VIMEFUNGASHWA KATIKA KIJIJI CHA DOMONIKI.




Kiasi cha Vitunguu vilivyobaki  baada ya kupima ujazo unaotakiwa kwa mujibu wa sheria kwa ujazo wa gunia moja.


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe: Mhandisi  Jackson Masaka leo amefanya ziara ya kushtukiza katika kijiji cha  Dominic kwa ajili ya kukagua ujenzi wa soko la Vitunguu na kuchunguza ufungashaji wa vitunguu hivyo kwenye mifuko kabla ya kupelekwa sokoni ambapo amebaini udanganyifu mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wanapofika mashambani.

Akiwa katika shamba la Mkulima mmoja aliyejulikana kwa majina ya Richard isaya, Mhe: Masaka ameshuhudia mfanyabiashara mmoja akiwa anapakia vitunguu ambavyo ameviweka kwenye ujazo wa zaidi ya Kilo 130 kwa gunia kinyume kabisa na sheria na taratibu za ufungashaji wa mazao ya Vitunguu ambapo mnunuzi anapaswa kufungasha ujazo wa Kilo 100 hadi 105 kama vitunguu hivyo vitakuwa havijakauka vizuri.

“Sitaki kuingilia makubaliano ya bei mliyokubaliana lakini sipo tayari kuona Mkulima akikandamizwa kiasi hiki kwa sababu ametumia nguvu, fedha na muda mwingi  mpaka kufikia hatua ya kuvuna na pia utaratibu huu unaifanya halmashauri kupoteza mapato kwa kiasi kikubwa sana” Amesema Masaka.

Mhe: Masaka ameongeza kuwa kila mfanyabiashara anayeingia katika Wilaya ya Mkalama ni lazima afuate sheria ndogondogo na taratibu zilizowekwa katika Wilaya hiyo na kamwe asilinganishe taratibu za Mkalama na maeneo mengine kwa sababu kila Wilaya ina Mkuu wake wa Wilaya na ana utaratibu wake wa kuongoza.

Kufutia tukio hilo, Mhe: Masaka aliagiza vitunguu hivyo vitolewe kwenye mifuko hiyo na kupimwa upya katika ujazo unaokubalika kisheria  na mfanyabiashara huyo alipe ushuru hapo hapo shambani kabla hajasafirisha mazao yake.

Naye Meneja wa wakala wa Vipimo  Mkoa wa Singida, Bw. Albogast Kajungu amesema kuwa ufungashaji wa mazao kwa kutumia mifuko ya aina yoyote tofauti na gunia la katani ni kinyume na sheria na kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika hivi karibuni kutenda kosa hilo hakumuweki hatiani mfanyabiashara pekee bali mpaka dereva anayesafirisha mazao  hayo.

“ Lakini pia wakulima waepuke kupima mazao yao kwa kutumia vifaa vya plastiki kama vile ndoo na visado kwa sababu vyombo hivyo vikipata joto hutanuka na kuongeza ujazo wa mazao jambo ambalo ni udanganyifu na kinyume na sheria ya ufungashaji mazao” Alimalizia Kajungu.

Ni kwa muda mrefu hivi sasa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wamekuwa wakiwaruhusu wafanyabiashara kufungasha mazao shambani kwa kutumia nyavu huku wafanyabiashara hao wakidai kutumia chombo kingine kinyume na hapo kunawakosesha soko hasa wanaposafirisha mazao hayo katika nchi za jirani kama Kenya na Uganda.


No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA