Tuesday 30 May 2017

Mkalama itajengwa na wanamkalama wenyewe- Masaka

Sehemu ya Viongozi waandamizi na wajumbe wa Umoja wa wakazi wenye asili ya Wilaya za  Iramba na Mkalama (IDA) wakimsikiliza mgeni rasmi wa hafla ya kukabidhi msaada wa Jezi Mhe: Mhandisi Jackson Masaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mapema mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka akizungumza na uongozi na wajumbe wa Umoja wa wakazi wenye asili ya Wilaya za Iramba na Mkalama (IDA) walipofika kwa ajili ya kutoa msaada wa jezi za timu ya Wilaya itakayoshiriki michezo ya Umitashumta ngazi ya Mkoa hivi karibun.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi  Godfrey Sanga akizungumza na uongozi na wajumbe wa Umoja wa wakazi wenye asili ya Wilaya za Iramba na Mkalama (IDA) walipofika kwa ajili ya kutoa msaada wa jezi za timu ya Wilaya itakayoshiriki michezo ya Umitashumta ngazi ya Mkoa hivi karibuni.


Katibu Mwenezi wa Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama daktari Alfred Mdima (Kushoto) akimkabidhi jezi Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhandisi Godfrey Sanga, Afisa Elimu Msing Bw. Chacha Kehogo na Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Joseph Nsoza (kulia).

     

Viongozi na wajumbe wa Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama (IDA) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka baada ya kukamilika kwa hafla ya kukabidhi jezi za timu ya Wilaya inayoshiriki michezo ya Umitashumta ngazi ya Mkoa.


Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama (IDA) umetoa msaada wa jezi pea mbili kwa timu ya Wilaya ya Mkalama inayotarajia kushiriki  mashindano ya Umitashumta katika ngazi ya Mkoa.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka  ambaye pia ndo alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi, aliwashukuru wajumbe wa umoja huo kwa uzalendo waliouonesha kwa timu hiyo na kuongeza kuwa si rahisi kwa watu walioondoka katika maeneo yao ya asili kukumbuka kupeleka misaada katika maeneo yao.

“Binafsi kwa kuteuliwa tu kuwa Mkuu wa Wilaya tayari nimeshakuwa mwanachama wa Umoja huu ndio maana nahakikisha Wilaya ya Mkalama inasonga mbele katika Nyanja zote” Alisema Masaka.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga ametoa rai kwa watu wengine kuiga mfano uliooneshwa na Umoja huo na kuongeza kuwa wamefanya jambo la kizalendo sana na linalopaswa kuenziwa.

“ Tunaomba msiishie hapa tu bali tuendelee kushirikiana katika kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Mkalama” Aliongeza Sanga.

Naye Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Joseph Nsoza alisema kuwa amefarijika sana kwa jinsi Wilaya ya Mkalama ilivyopiga hatua hali ambayo ni tofauti kabisa na kipindi walipokuwa wanaondoka na kuupongeza uongozi wote wa Wilaya kwa kazi ngumu ya kuhakikisha Mkalama inazidi kuwa bora kila siku.

“ Wakati tunaondoka hapa nyumbani palikuwa nyuma sana kimaendeleo lakini leo hii tumekuja na kuikuta Mkalama yetu mpya kabisa na inayozidi kuendelea, tumefarijika sana kwa hili” Alisema Nsoza.

Nsoza alimaliza kwa kuahidi kuutumia umoja huo kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo na kwamba malengo ya Umoja huo na ya Wilaya yanalingana.



No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA