Sunday, 1 May 2016

IRAMBA WAFANYA HARAMBEE KWA MAFANIKIO

Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe: Allan Kiula(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai wakifuatilia namna zoezi la harambee linavyoendelea.

Mbunge viti maalum (CCM) kutoka jimbo la Kaskazini Unguja Mhe: Anjelina Adam Malembeka akicheza Muziki na wanawake waliofika kwenye harambee hiyo.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Christopher Ngubiagaia akionesha kiasi cha Shilingi Milioni Moja kilichotolewa na Mh: Anjelina Adam Malembeka (hayupo pichani) kama sehemu ya mchango wake kwenye harambee hiyo.

Mh: Anjelina Adam Malembeka akifurahia jambo wakati wa zoezi la harambee hiyo.

Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe:Allan Kiula akizungumza na wananchi na wadau waliofika kwenye harambee hiyo.

Mgeni rasmi katika harambee hiyo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Christopher Ngubiagai akitoa hotuba yake kabla ya kuhitimisha zoezi la harambee hiyo.

Baada ya harambee ya kuchangia madawati yenye mafanikio iliyofanyika katika Wilaya ya Mkalama, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambaye pia ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mheshimiwa Christopher Ngubiagai alifanikiwa kuongoza harambee nyingine kama hiyo akiwa kama Mgeni Rasmi iliyofanyika katika Wilaya ya Iramba jumamosi aprili 30.

Huku akitokea katika zoezi la usafi kitaifa, Ngubiagai alionesha kufurahishwa na umoja na mshikamamo uliooneshwa na wananchi wa Iramba katika zoezi hilo wakiongozwa na Mbunge wao Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ambaye aliwakilishwa na Mbunge wa jimbo la Mkalama, Mheshimiwa Allan Kiula.

Jambo la kuvutia Zaidi katika harambee hiyo ni uwepo usiotarajiwa wa Mbunge wa Viti maalum jimbo la Kaskazini Unguja Mheshimiwa Anjelina Adam Malembeka ambaye alinogesha Zaidi harambee hiyo kwa kusimama na kucheza muziki na wanawake wenzake wote waliokuwepo ukumbini hapo.

Kabla ya kusimama kucheza muziki huo, Malembeka alitoa kiashi cha shilingi elfu hamsini  kama ishara ya kufungua muziki huo na mara baada ya kumaliza kucheza alitoa kiasi cha Shilingi milioni moja kama sehemu ya mchango wake katika harambee hiyo.

Akizungumza kabla hajatoa kiasi hicho, Malembeka alisema kuwa yeye ni mdau mkubwa wa Elimu na hata Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alipomuomba kushiriki harambee hiyo hakusita hata kidogo.

“Mheshimiwa Nchemba aliniambia kuhusu harambee hii, nilimhakikishia kuwa lazima nije” Alisema Malembeka huku akishangiliwa na umati wa watu uliokuwepo ukumbini hapo.
Naye Mbunge wa Mkalama Mheshimiwa Allan Kiula alisema kuwa amefarijika sana na uandaaji wa tukio hilo na kuongeza kuwa tatizo la Iramba ni tatizo la Singida yote hivyo yeye kama Mbunge na Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Singida alipokea ombi la Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kama agizo.
“Lakini nisisitize wazazi tuwe na desturi ya kutembelea shule wanazosoma watoto wetu ili kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili likiwemo hili la madawati na miundombinu mibovu”

Akihitimisha zoezi hilo, Mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mheshimiwa Christopher Ngubiagai, aliwashukuru na kuwapongeza wote waliofika katika harambee hiyo huku akiwaomba na kuwasisitiza waendelee na moyo huo huo wa kizalendo katika Nchi yao na waendelee kuunga Mkono Juhudi za Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli.

“Leo watu wa Iramba mmeweka historia kubwa sana katika maisha yenu na vizazi vijavyo na kwa elimu bora watakayopata wanafunzi watakaokalia madawati hayo, itakuwa ni sehemu ya baraka kubwa na nyingi mtakazozipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Ahsanteni sana” Alisema Ngubiagai.

Katika harambee hiyo jumla ya shilingi Milioni 35 laki nne na elfu 65 ikiwa ni pesa taslimu zilikusanywa huku ahadi ya jumla ya shilingi Milioni 50 na madawati 600 ikitolewa katika kuhakikisha tatizo la ukosefu wa madawati katika Wilaya ya Iramba linabaki kuwa historia.

1 comment:

  1. Sasa naanza kuwaelewa, Sijui tulikuwa wapi siku zote. Asanteni kwa kusaidia wadogo zangu.

    ReplyDelete

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA