Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega akifungua kikao cha baraza la Madiwani mapema leo |
Waheshimiwa madiwani na Wakuu wa Idara wakiwa katika kikao cha baraza la Madiwani mapema leo |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza machache wakati wa kikao cha baraza la madiwani mapema leo |
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
limefanyika leo huku hoja mbalimbali zikiibuliwa na kupatiwa majibu.
Baraza hilo ambalo ni la kwanza kwa Mwaka wa Fedha
2017/2018 liliipa kipaumbele sekta ya Elimu na Kilimo ambapo madiwani
walielezea hali ya utekelezaji katika sekta hizo na changamoto zinazopatikana kutoka kwenye kata zao huku pia wakiainisha
mikakati mbalimbali waliyojiwekea kukabiliana na changamoto hizo.
Moja ya hoja zilizoibuliwa katika baraza la leo ni
changamoto zilizojitokeza katika zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya
Taifa ambapo katika baadhi ya vijiji mashine zimeshindwa kusoma alama za vidole
za baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha.
Akijibu juu ya hoja hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Godfrey Sanga amekiri kupokea
taarifa za kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amewatoa hofu wananchi hao kwa
sababu mamlaka husika inaendelea
kushughulikia suala hilo na pindi likipatiwa ufumbuzi wananchi hao wataarifiwa.
Diwani wa Kata ya Ilunda Mhe. Mohamedi Imbele alitaka
kujua mipango na mikakati ambayo Halmashauri imeweka ili kuhakikisha kunakuwepo
na maadhimisho ya Wilaya ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji maarufu kama Nane Nane ambapo Makamu
Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Mhe. Erasto Linza
alimhakikishia Mhe. Imbele na Wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuwa mipango
ya kuhakikisha sikukuu hiyo inaadhimishwa ngazi ya Wilaya inaendelea vizuri na
hatua iliyobaki ni kupanga Sehemu ambayo maadhimisho hayo yatafanyika kwa Mwaka
ujao.
Suala la utunzaji wa vyanzo vya maji lilikuwa ni moja ya
mambo yaliyoibuliwa katika baraza hilo ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega alitoa msimamo wa Halmashauri ya Wilaya
kuwa kuanzia sasa gharama za kurejesha huduma ya maji katika kijiji ambacho watu wake watahujumu vyanzo na miundombinu
ya Maji zitatolewa na kijiji husika na si halmashauri.
Baraza hilo hutanguliwa na baraza la Kata ambapo waheshimiwa
madiwani hupokea majibu ya wataalam kuhusu changamoto mbalimbali zilizopo
kwenye kata zao na kuziwasilisha kwa wataalam kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment