Wednesday, 16 March 2016

MKUU WA SHULE YA SEKONDARI CHEMCHEM ATUMBULIWA


 Baada ya malalamiko ya muda mrefu ya Wananchi dhidi ya mkuu wa shule ya sekondari ya Chemchem iliyopo Wilayani Mkalama bwana Juma Kokoro, hatimaye Mkuu wa Wilaya Hiyo bw. Christopher Ngubiagai (aliyesimama pichani hapo juu) ameagiza kusimamishwa kazi mkuu huyo wa shule, akamatwe  na uchunguzi dhidi yake ufanyike ili akipatikana na hatia hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Kwa mujibu wa wanafunzi wa shule hiyo, mwalimu huyo amekuwa akiwarubuni wanafunzi hao na kuwataka wambusu ndipo aweze kusikiliza matatizo yao pindi wakienda ofisini kwake.

Mkuu huyo alitoa agizo hilo leo alipozungumza na watendaji na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama juu ya masuala mbali mbali yanayoikabili wilaya hiyo likiwemo suala la Ulinzi na usalama, ujenzi wa mabweni ya sekondari kwa wanafunzi wa kike, upatikanaji wa chakula cha kutosha Wilayani hapo pamoja na kusisitiza utekelezaji wa agizo la Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa John Pombe Magufuli kuwa vijana wote kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni hawapaswi kuonekana wakizurula wala kucheza mchezo wa pool badala yake wakafanye kazi za kuliletea taifa maendeleo.

Kuhusu hilo, Mkuu wa wilaya amewaagiza viongozi hao wote kutimiza wajibu wao na kutumia mamlaka waliyonayo kusimamia agizo hilo  na endapo watapatikana vijana wakicheza mchezo wa pool au wakiwa wamekaa tu bila shughuli maalum, mtendaji wa eneo husika atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

PICHA CHINI NI VIONGOZI NA WATENDAJI WA HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA WAKIMSIKILIZA MHESHIMIWA MKUU WA WILAYA.







No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA