“Elimu ni moyo wa uhakika na hakikisho la uhai wa
maendeleo endelevu ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla”
Hayo ni maneno yaliyotamkwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida
Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho
ya Juma la Elimu tukio lililofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Nchimbi ambaye alimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo,
alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote wa elimu chini ya mwamvuli wa
Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) ambapo aliwataka watumie maadhimisho ya
mwaka ujao kutoa majibu ya tathmini ya utekelezaji wa changamoto zote
walizoziona katika Wilaya za Nanyumbu na Mkalama.
“Haiwezekani kila mwaka muwe mnazungumzia changamoto za
aina moja hivyo ni lazima muweke mpango mzuri wa kufanya ufuatiliaji wa karibu
wa utekelezaji wa changamoto zote mlizoziainisha” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi aliushukuru uongozi na wananchi wa Mkalama
kwa ujumla kwa kuahidi kubadilisha matokeo waliyoyapata mwaka jana ambapo
aliwasisitiza wajikite zaidi kwenye mabadiliko ya vitendo badala ya maneno.
Kabla ya kutangaza kufunga maadhimisho ya juma la Elimu
kwa mwaka huu, Mhe. Nchimbi aliendesha harambee ya kuchangia elimu Wilayani hapa
ambapo jumla ya shillingi 600,000 zilipatikana.
Awali akizungumza maneno machache kabla ya kumkaribisha
mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka alisema
kuwa TenMet waliamini Mkalama bado ipo hai ndio maana walifika kuisaidia
kuainisha sababu mbalimbali zilizosababisha kutokuwa na matokeo mazuri ambapo
aliwaahidi kuwa Wilaya yake haitofanya vibaya tena.
Wakati huo huo Mhe. Masaka alitumia fursa hiyo kuwatakia kila
la kheri waislam wote wa Wilaya ya Mkalama katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani ambapo aliwataka wafanyabiashara wote Wilayani hapa kutopandisha bei
za vyakula ambavyo hutumiwa kama futari na daku katika kipindi hiki.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itafuatilia kwa
karibu sana utekelezaji wa agizo hili na atakayekiuka hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake” Aliongeza Mhe. Masaka.
No comments:
Post a Comment