Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akihutubia wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo. |
Wajumbe mbalimbali waliojitokeza akihutubia wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo
ameongoza kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ambapo katika hotuba yake ametoa maelekezo
mbalimbali kwa wadau na idara mbalimbali zilizopo Wilayani Mkalama.
Kikao hicho mbali na kuhusisha baraza lote la Madiwani,
pia kilihusisha taasisi mbalimbali zinazoendesha shughuli zake Wilayni Mkalama,
Watendaji wote wa kata, wawakilishi wa taasisi za dini na wawakilishi wa
vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.
Mhe. Masaka aliwataka wananchi na viongozi kutambua
umuhimu wa wingi wa fedha zinazotolewa na serikali katika kuhudumia Eimu nchini
kwa kuhimiza watoto kwenda shule, walimu kufanya kazi pindi wawapo shuleni na
wazazi kuonesha mwamko wakati wa kuchangia huduma mbalimbali za uboreshaji wa
Elimu za watoto wao.
“Jambo la pili nitumie fursa hii kuhimiza wakulima wote
walime mazao ya mkakati ambapo kwa Wilaya yetu mazao hayo ni pamba, korosho,
alizeti na Vitunguu” Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alisisitiza kuwa ili kilimo cha Mkakati kiweze
kuwa na tija ni lazima wakulima watumie mbegu bora, wapande mazao yao kwa
vipimo sahihi na watumie vipimo stahili katika uwekaji wa dawa za kuua wadudu
wanaoathiri mazao hayo.
“Mawakala wa huduma za Misitu nchini (TFS) na idara ya
Maliasili ni lazima waonekane wapo badala ya kuziachia serikali za vijiji kesi za uvamizi wa maeneo ya misitu ingawa
pia vijiji vyote vinapaswa kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya misitu”
Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alitumia fursa hiyo kusisitiza wananchi wajenge
viwanda vidogo kama viwanda vya kukamua
mafuta ya Alizeti na kuagiza kila mtu awaunge mkono wenye viwanda hivyo ili
wafanikiwe na hatimaye waweze kufungua viwanda vikubwa.
“Sio Afisa afya anaenda kukagua kiwanda na kukuta
mazingira yasiyoridhisha lakini badala ya kushauri namna ya kuboresha mazingira
hayo anaamua kuchukua uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho” Alisisitiza Mhe.
Masaka.
Katika hotuba yake
Mhe. Masaka pia alizitaka taasisi zote
zinazofanya shughuli zake Wilayani Mkalama kuwa na mipango yenye mwelekeo mmoja
ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za msingi kwa wakati badala ya
huduma moja kusubiri uwepo wa huduma nyingine.
“Sio Tarura wanajenga barabara Kinyambuli, Halmashauri
inaenda kujenga kituo cha Afya Gumanga, Tanesco wanapeleka umeme Kinyangiri na
Idara ya Maji wanapeleka maji Ibaga, hapo mtakuwa hamjamsaidia mwananchi kwa
sababu hata mkimpelekea kituo cha Afya kizuri, kama hakuna barabara nzuri
kufika kwenye kituo hicho au umeme wa kutumia kituoni hapo itakuwa ni kazi bure”
Alisema Mhe. Masaka.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Masaka aliwaomba wananchi
na taasisi za dini zilizopo wilayani Mkalama kuisaidia serikali kwa kutoa
maeneo ambayo hawayatumii ili yatumike katika shughuli za Maendeleo.
“Msiishie tu kumiliki maeneo hayo bila kuyaendeleza kwa
kufanya shughuli za Maendeleo hivyo kama ni kilimo limeni, kama ni viwanda
wekeni viwanda na kama mlipanga kuweka taasisi za Elimu wekeni taasisi hizo”
Alimalizia Mhe. Masaka.
No comments:
Post a Comment