“Kama umeshindwa kumsikiliza mama yako mzazi aliyekuzaa,
utanisikiliza mimi Mkuu wa Wilaya?”
Hilo ni swali alilouliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe.
Mhandisi Jackson Masaka leo wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ambayo katika ngazi ya Wilaya yamefanyika katika kijiji
cha Iguguno.
Mhe. Masaka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho
hayo aliuliza swali hilo wakati akiwasisitiza wananchi wa Wilaya ya Mkalama
kujenga utamaduni wa kumaliza matatizo yao wenyewe badala ya kusubiri viongozi
wa serikali waingilie kwenye matatizo hayo.
“Ni aibu kwa watu wa familia moja kutegemea watendaji wa
serikali kumaliza migogoro yao hivyo ni lazima kila mwananchi kwa nafasi yake
ahakikishe anashiriki kikamilifu katika kutatua migogoro inayomkabili ndani ya
familia yake” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka aliongeza kuwa kama matatizo hayo yataonekana
kuzidi uwezo wa familia husika, ni vizuri hatua stahili za kushughulikia
matatizo hayo zikafuatwa kwa kuanza kuyafikisha serikali ya kijiji, kata na tarafa
kabla hayajafika katika ofisi yake.
Akitoa ujumbe wa maadhimisho ya Muungano ya Mwaka huu Mhe.
Masaka amewataka wananchi kuhakikisha wanadumisha na kuuenzi Muungano huo huku
akiwataka kupuuza kauli za baadhi ya watu wachache wanaobeza
faida kubwa zinazopatikana ndani ya pande zote mbili za Muungano huo.
“Wewe Mwananchi wa Lukomo au Nyeri, una mashamba yako na umepata
mazao ya kutosha, inakusaidia nini kuhoji kwanini Rais wa Zanzibar naye anapanda ndege?” Aliuliza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka aliwasihi wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama
kuhakikisha wanalinda na kuitunza amani na utulivu uliopo hivi sasa huku
akikisisitiza kuwa serikali haitafumbia macho aina yoyote ya viashiria vya
uvunjifu wa amani vitakavyoonekana na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa
wahusika wote watakaoonesha viashiria hivyo.
Kuhusu kampeni ya kitaifa ya chanjo ya kujikinga na
saratani ya Mlango wa kizazi inayoendelea hivi sasa kwa wasichana wenye umri wa
miaka 14 Mhe. Masaka amewataka wazazi wote kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata
chanjo katika vituo vitakavyotajwa ili kuwaepusha wasichana hao na tatizo hilo
ambalo linazidi kuwa kubwa kila Mwaka.
“Kila Mwaka saratani ya mlango wa kizazi husababisha vifo
vya wanawake zaidi ya 2000 nchi nzima hivyo asitokee mzazi yoyote kumkataza mwanae
kupata chanjo hiyo kisa yeye hakuwahi kupatiwa kwa sababu miaka inabadilika na
tatizo hili linazidi kuwa kubwa ndio maana Serikali imeamua kuchukua hatua”
Alisisitiza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alimalizia hotuba yake kwa kuwasihi wananchi
kuendelea kuunga mkono juhudi zinazooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli ambapo pia aliwataka waendelee
kumuombea afya njema ili aendeleze jitihada za kuhakikisha Tanzania Mpya
inasonga mbele.
Tafadhali Bonyeza hapa ili uweze kumuona Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati akihutubia leo.
No comments:
Post a Comment