Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo (Wapili kutoka kulia) akielekea kwenye kinu cha kuchenjulia Madini katika Mgodi wa Tumuli mapema leo. |
Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo juu ya namna kazi inavyofanyika katika Mgodi wa Tumuli Mapema leo. |
Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika kata ya Tumuli mapema leo. |
Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akizungumza na wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Tumuli (Hawapo pichani) alipofanya Ziara katika Wilaya ya Mkalama mapema leo. |
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akitambulisha Wataalam alioambatana nao wakati wa Ziara ys Naibu Waziri wa Mdini Mhe. Stanslaus Nyongo. |
Mwenyekiti wa Hlmashauri ya Wilaya ya Mkalama akitoa neno la Shukrani kwa Naibu Waziri wa MadiniMhe. Stanslaus Nyongo alipomaliza kuzungumza na Waachimbaji wadogo. |
Katika muendelezo wa ziara za viongozi wakuu mbalimbali wa
serikali ya Awamu ya Tano Wilayani Mkalama leo ilikuwa ni zamu ya Naibu waziri
wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye alifika katika kata ya Tumuli kwa ajili
ya kusikiliza na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Mgodi wa madini ya dhahabu uliopo
kwenye kata hiyo ambao unaohusisha Wachimbaji wadogo na mwekezaji mwenye uraia
wa China.
Mara baada ya kufika Shule ya Msingi Tumuli ambako ndipo
alipofanyia Mkutano baina yake na Wachimbaji hao wadogo Mhe. Nyongo aliwataka
viongozi wa Chama cha Wachimbaji hao kumueleza kwa kina mchakato mzima wa suala
hilo mpaka kufikia katika hatua ya Mgogoro.
Akielezea mchakato mzima ulivyokuwa mmoja wa viongozi wa
wachimbaji hao Bw. Salum Kapalale alisema kuwa wachimbaji wote wadogo waliopo
katika kata hiyo walikuwa wanamiliki jumla ya maduara 90 huku yakitoa fursa ya
ajira kwa watu 1243 kabla ya Mzawa mmoja akishirikiana na mwekezaji kufika na
kuwaondoa katika maeneo yao.
“Tangu tumeanza uchimbaji wa Madini mnamo mwaka 2007, eneo
la Mgodi lilikuwa wazi mpaka ulipofika mwaka 2010 ambapo mtu anayefahamika kwa
majina ya Salum Kondo alifika na kudai kuwa yeye ni mmiliki wa eneo lote la
uchimbaji ambapo baada ya kuzungumza naye tulikubaliana kushirikiana naye
katika shughuli za uchimbaji” Aliongeza Kapalale.
Kwa mujibu wa Kapalale hali ya taharuki iliendelea kutanda
mwaka 2012 baada ya mwananchi mmoja aliyetambulika kwa majina ya Ibrahim Sadof Shakama
kufika katika eneo hilo la Mgodi na kudai kuwa eneo hilo ni la marehemu baba yake
mzazi hivyo aliwataka wachimbaji hao wampe eneo hilo ili ampe mwekezaji
Mkubwa ambaye mbali na kuwalipa fidia
wachimbaji hao, pia watapata ajira katika Mgodi huo watasaidia kujenga
miundombinu mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo kabla hawajaanza shughuli
za uchimbaji wa madini hayo.
Kufuatia makubaliano hayo wachimbaji hao walikubali
kumuachia Bw. Shakama eneo hilo huku wakisubiri kutekelezewa makubaliano yao
jambo ambalo halikufanyika kabisa na badala yake waliishi bila ajira yoyote
kuanzia Mwaka 2012 mpaka Mwezi Juni 2016 ambapo
Mwekezaji mwenye Uraia wa China alifika na kuanza kazi Mgodini hapo na walipojaribu
kumfuata Bw. Shakama kuhusu makubaliano yao ya awali aliwajibu kuwa wao ni
wachimbaji wadogo hivyo hawatambuliki.
“Jibu hili lilituvunja moyo sana na ndipo tulipoanza
kuchukua hatua mbalimbali za kudai haki yetu ambapo aliyekuwa Waziri wa Nishati
na Madini Mhe. Sospeter Mhongo alifika hapa na baada ya kusikiliza pande zote
alitoa siku 7 kwa Uongozi wa Wilaya kuhakikisha umemalizika ambapo baada ya
Mhe. Waziri kuondoka Mhe. Mkuu wa Wilaya
pia alitoa siku 14 kwa mwekezaji huyo kuhakikisha amelipa fidia yote anayodaiwa
jambo ambalo halijatekelezwa mpaka leo” Aliongeza Kapalale.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan
Kiula mbali na kumshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kukubali wito wake na kufika
katika eneo hilo, Alimtaka Kamishna wa Madini wa kanda ya kati kuhakikisha
anatimiza wajibu wake ipasavyo kwani migogoro mingi ya madini Wilayani
hapa inatokana na ofisi yake kutosimama
imara.
“Mhe. Naibu Waziri Namuomba sana Kamishna wa Madini kanda
ya kati atusaidie sana katika mambo kama haya kwa sababu ninaamini kama akiivaa
taaluma yake ipasavyo hatutafikia katika hatua ya Migogoro ya aina hii ambayo
kama wananchi wa Mkalama wangekuwa ni wakorofi basi kungekuwa na maafa makubwa
sana hapa” Alisema Mhe. Kiula.
Mhe. Kiula alimalizia kwa kuwapongeza wananchi hao kwa
Utulivu Mkubwa walioanao wakati wa migogoro na wawekezaji ambapo
aliwahakikishia kuwa atakuwa nao bega kwa bega kwa kuwaletea viongozi husika
katika kila jambo linalowaletea vikwazo vikubwa kwenye Maendeleo yao.
Akizungumza mara baada ya kupata picha kamili ya mgogoro
huo, Mhe. Nyongo alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na wajanja wachache wanaojua
taratibu na sheria ambao bila kupitia ngazi za viongozi husika wanapitisha
baadhi ya mambo ambayo baadae hugeuka kuwa mateso kwa wananchi wa kipato cha
chini.
Mhe. Nyongo aliongeza kuwa hata majibu ya dharau ya kiburi
yanayotolewa kwa wananchi kutoka kwa wawekezaji hao yanatokana na wawekezaji
hao kujua fika kuwa sheria itawalinda pindi wananchi hao watakapowashtaki.
“Sasa mimi nisiseme maneno mengi, ninajua hata nikitoa
siku ngapi maagizo yangu hayatotekelezwa hivyo ninasimama na wananchi wangu
kudai haki yao na sina haja ya kupoteza Muda, Hivyo Mhe. Kamishna wa Madini
fanya mpango Keshokutwa wakati napita hapa
nionane na hao watu watatu ambao ni Ibrahim, Salum na huyo Mwekezaji nibanane nao ili
wanapokuja kwenye kikao cha tar 19 waje na jibu lililonyooka” Aliagiza Mhe.
Nyongo.
Mhe. Nyongo Alisisitiza
kwa kutoa onyo kwa watu wote wenye ujanja wa aina hiyo kuacha mara moja
kwani serikali hii hairuhusu hata kidogo matumizi ya njia za mkato katika
kudhulumu haki za wananchi wanyonge.
“ Kwenye serikali hii ya Mhe. John Magufuli ubabaishaji hauna
nafasi hata kidogo hivyo asipowalipa haki zenu tutasimamisha mradi wake”
Alimalizia Mhe. Nyongo.
No comments:
Post a Comment