PICHA 10 CHINI: Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Joseph Kakunda akisalimiana na viongozi na wakuu wa idara mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi wa Maji wa Iguguno.
Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda (katikati) akisisitiza jambo mara baada ya kuona zoezi la uchimbaji wa kisima kikubwa cha maji katika kata ya Nduguti (kama inavyoonekana nyuma yao) Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga. |
“Hongereni kwa kuwa na mradi mkubwa wa maji ambao kwa
hakika umewaongezea uwezo mkubwa wa kutoa huduma ya maji katika maeneo yote
yanayozunguka kata ya Iguguno”
Hayo ni maneno
yaliyotamkwa na Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Joseph Kakunda mara baada ya kufika katika kituo cha Kutolea huduma za maji kilichopo
katika kata ya Iguguno wakati wa ziara
yake ya Kikazi ya siku moja aliyoifanya Wilayani Mkalama mapema leo hii.
Ziara hiyo ya Mhe. Kakunda ilihusu ufuatiliaji wa utoaji wa huduma mbalimbali za
jamii Wilayani hapa huku ikijikita zaidi katika sekta ya maji na Elimu ambapo
mbali na kutembelea Kituo hicho Kikubwa cha Maji kilichopo katika kata ya
Iguguno, pia alifika katika katika Shule ya sekondari ya Iguguno na kujionea
miradi mikubwa iliyojengwa na serikali kupitia mafundi wa kawaida kwa utaratibu
unaojulikana kitaalam kama ‘’Force Account’’.
Akiwa shuleni hapo Mhe. Kakunda alisifu ubora wa miradi
hiyo inayojumuisha Madarasa 8, Mabweni mawili, Vyoo vyenye matundu 11, bwalo la
chakula na Maabara ambapo vyote kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi milioni
416 tu ikiwa ni chini ya robo ya gharama ambazo zingetumika kupitia utaratibu wa Wakandarasi na wazabuni.
Kutokana na ubora wa miradi hiyo, Mhe. Kakunda alitumia
nafasi hiyo kuziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatumia mafundi wa
kawaida (local fundi) katika miradi yote midogo hasa ile inayohusu ujenzi wa
madarasa, mabweni, vyoo, daharia n.k ambapo
alisisitiiza matumizi ya wakandarasi yawe ni kwenye miradi mikubwa tu.
Moja ya mambo yaliyoonekana kutomfurahisha Mhe. Kakunda katika
ziara hiyo ni idadi kubwa ya wanafunzi wa kike waliokatishwa masomo yao
kutokana na kupewa ujauzito ambapo Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama Bw. Fredi Kimeme alitaja idadi ya wanafunzi 12 waliokatishwa masomo yao kutokana
na kupewa ujauzito tangu Mwezi Januari Mpaka sasa.
Kuhusiana na hilo, Mhe. Kakunda alitoa rai kwa wazazi na
walezi wote nchini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kukomesha suala
hilo huku akiainisha mbinu ambayo inatumiwa na wazazi wengi kwa kufanya makubaliano
na wahusika wa mimba hizo ili waepukane na kifungo cha miaka 30 jela jambo
ambalo limesababisha kesi nyingi kutoripotiwa na zile zilizoripotiwa kufutwa
kutokana na shahidi namba moja (Mjamzito) kukana uhusika wa mtuhumiwa juu ya
ujauzito huo.
Hata hivyo Mhe. Kakunda alielezea dhamira ya Wizara yake kupeleka
hati ya dharula bungeni ili itungwe sheria itakayofuta dhamana kwa mtu
anayetuhumiwa kumpa ujauzito Mwanafunzi ambapo pia utafanyika ufuatiliaji na uchunguzi kwa
kila Mwanafunzi aliyepewa ujauzito mpaka atakapojifungua kisha mtoto huyo atapimwa
DNA ili kuthibitisha kama mtuhumiwa ndiye baba wa mtoto au la.
Awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mbunge wa
jimbo la Mkalama Mhe. Alan Kiula alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili
Wilaya hiyo huku suala la ukosefu wa hospitali ya Wilaya na upungufu wa
watumishi hasa katika sekta ya Elimu ya Afya likionekana kupewa kipaumbele
zaidi ambapo Mhe. Kakunda aliwahakikishia viongozi, Watumishi na wananchi wote
wa Wilaya ya Mkalama kuwa Serikali imeshaweka katika mipango yake suala la
ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Wilaya na kwamba halmashauri inapaswa
kukamilisha taratibu za awali tu ikiwemo upatikanaji wa eneo la kutosha kwa
ajili ya ujenzi huo.
“Hili la upungufu wa watumishi hasa walimu nalichukua na
nawaahidi katika mgao huu wa Mwezi Desemba hadi januari tuwaangalia kwa jicho
la pekee kabisa” Alihitimisha Mhe. Kakunda.
No comments:
Post a Comment