|
|
Pongezi kubwa zimetolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama kufuatia kupata hati safi kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe:
Rehema Nchimbi wakati wa kikao cha kujadili hoja mbalimbali zilizoainishwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kilichojumuisha Mkuu wa Wilaya
hiyo, madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri na
Wataalam wa idara mbalimbali katika Wilaya hiyo.
“Sina wasiwasi na Wilaya ya Mkalama kwa sababu inaongozwa
na Wahandisi katika nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya na ndio maana kazi zote zilizofanyika katika Wilaya hii zimefanyika kitaalam”
Alisema Mhe: Nchimbi.
Mhe: Nchimbi alisema kuwa jambo hilo limeifanya
halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuwa na sifa ya kipekee ukilinganisha na
Wilaya nyingine kwa sababu changamoto inayoyakabili maeneo mengi ni ukosefu wa
wahandisi hali inayosababisha kila mradi kutotekelezwa kitaalam.
“BOQ ya mwanzo ya jengo hili haikuwa na sura nzuri lakini
Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya waliweka taaluma zao hapa tena bila kulipwa na
kutengeneza BOQ ambayo imelifanya jengo hili kuwa la mfano katika Ofisi
zilizojengwa kwa fedha ya serikali” Aliongezea Mhe: Nchimbi.
Katika hatua nyingine Mhe: Nchimbi ameagiza kukarabatiwa
kwa boma la Mkalama lililokuwa likitumiwa na Serikali ya Ujerumani wakati wa
Ukoloni na hatimaye liweze kutumika kama chanzo cha mapato ya Halmashauri.
“ Naomba Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Wataalam wako mkishirikiana
na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali mkae chini na mniletee andiko litakaloonesha
ni jinsi gani mnaweza kulifanya boma hili kuwa chanzo cha mapato ya Halmashauri
ya Wilaya na andiko hilo nilipate Agosti
28 mwaka huu” Alimalizia Mhe: Nchimbi.
Kumsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida bonyeza hapa.
No comments:
Post a Comment