Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa
kusimamishwa kazi watumishi wenye tuhuma mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha
au mali ya umma nchini, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Christopher
Ngubiagai leo ameagiza kurejeshwa kwa mtumishi aliyestaafu ili aje ajibu tuhuma
zinazomkabili.
Mhe: Ngubiagai ametangaza uamuzi huo mbele ya Waandishi
wa habari ofisini kwake Wilayani Iramba kufuatia Udanganyifu na matumizi mabaya
ya madaraka katika fedha za halmashauri ya Wilaya hiyo kati ya mwaka 2013 na
2015 ambapo jumla ya shilingi 398,593,675 zimetumika bila idhini ya kamati ya
Fedha, Uongozi na Mipango na Baraza la Madiwani kama inavyoelekezwa chini ya
kanuni ya 42(3) ya kanuni za kudumu zinazoongoza Halmashauri ya Wilaya ambapo
fedha hizo ni za mwaka wa bajeti 2013/2014 na 2014/2015.
Kufuatia ubadhirifu huo, Mhe: Ngubiagai ameagiza mamlaka
husika kuwasimamisha kazi na kuwakabidhi kwenye vyombo husika watumishi watano
ambapo watatu kati yao walihamishiwa vituo vingine vya kazi, mmoja amestaafu na
mwingine bado ni mfanyakazi wa halmashauri
ya Wilaya hiyo.
Watumishi hao ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi. Halima Mpita ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa
halmashauri ya Mji Tunduma, aliyekuwa Afisa Utumishi wa Wilaya hiyo Tabia Nzowa
ambaye kwa sasa ni Afisa Utumishi wa Wilaya ya Kyela, aliyekuwa Afisa Mipango
wa Wilaya Hiyo Stephen Pundile ambaye kwa sasa ni Afisa Mipango wa Wilaya ya
Ulanga, Injinia Mstaafu wa Wilaya hiyo L.S.K Rweyemamu na Afisa Maendeleo ya
Jamii wa Wilaya hiyo mpaka sasa, Focus Marwa.
“Wale ambao walishahamishiwa vituo vingine vya kazi, taratibu
zinafanywa ili waweze kusimamishwa kazi huko na kurejeshwa kuja kujibu tuhuma
zao huku wakipisha uchunguzi wa kina utakaofanywa na vyombo husika dhidi yao”
Alisema Ngubiagai.
Mhe: Ngubiagai ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo alimalizia taarifa yake kwa kuwataka Wakuu wa
Idara, Viongozi na Watumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo Kutenda na
Kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni na misingi ya maadili ya Viongozi
wa umma na kwamba atakayefanya kinyume na hivyo atakuwa amejitafutia matatizo.
No comments:
Post a Comment