Bi Emeliana Mkoma ambaye ni moja wa walengwa wa Tasaf alipotembelewa nyumbani kwake jana. Picha Chini ndio nyumba aliyojenga kwa ruzuku ya Tasaf. |
Bi Leah Mpinga akiwa anazungumza na ujumbe wa Tasaf mara baada ya kufika nyumbani kwake jana. Picha Chini ni Mbuzi aliowanunua kutokana na ruzuku ya Tasaf. |
Mlengwa Bi Wampumblya Joseph akiwa na mwanae alipotembelewa na Ujumbe wa Tasaf Wilaya ya Mkalama jana. |
Hii ndio nyumba aliyokuwa akiishi Bi Wampumblya Joseph kabla ya kuingizwa kwenye mpango wa Tasaf. |
Na hii ndio nyumba aliyofanikiwa kujenga kupitia ruzuku anazopata kutoka Tasaf. |
Mfuko wa Mendeleo ya Jamii (TASAF) Wilayani Mkalama
umeendelea kuziwezesha kaya masikini ili kujikwamua kutoka katika hali waliyo
nayo.
Mapema kabla ya kuwawezesha wananchi wa vijiji vya Iambi
na Mwando, Ofisi ya Mfuko huo Wilayani Mkalama ilifanya tathmini ya kutambua na
kuangalia shughuli mbalimbali walizofanya baadhi ya walengwa kutokana na ruzuku
walizopewa awamu iliyopita.
Emiliana Mkoma ni mmoja wa walengwa wa Mradi huo kutoka
kijiji cha Mwando ambaye anasema kuwa mradi huo umemuwezesha kununua Mbuzi watatu,
Mabati sita ya kuezeka nyumba yake hali iliyomuondoa kwenye nyumba ya tembe
ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha ya familia yake hasa msimu wa mvua.
“Lakini pia ruzuku ya Tasaf imeniwezesha kuwasomesha
watoto wangu wawili ambao sikuwa na uhakika wa kuwaendeleza kimasomo hasa baada
ya kifo cha baba yao lakini namshukuru Mungu hivi sasa mmoja amemaliza darasa
la saba na mwingine amemaliza kidato cha nne, Hiyo yote imetokana na mchango
mkubwa wa Tasaf” Aliongeza Emiliana.
Mlengwa wa Pili alikuwa ni Leah Mpinga ambaye kutokana
na umri mkubwa alionao na maradhi yaliyokuwa yakimuandama mara kwa mara
ilimuwia vigumu kuweza kujihudumia lakini mara baada ya Tasaf kuanza
kumuwezesha amerejewa na matumaini na uhakika wa kupata huduma zote za msingi
anazohitaji.
“Nimefanikiwa kuutibu mguu wangu ambao ulikuwa
unakaribia kukatwa kutokana na maumivu makubwa niliyokuwa nayapata na jambo la
pili nimefanikiwa kununua Mbuzi ambao wanaendelea kuzaa hivyo nategemea kuwa na
mbuzi wengi sana siku za usoni” Aliongeza Bi. Mpinga.
Kwa upande wake bi Wankembeta Kingu ambaye kwa sasa
amezeeka sana kiasi cha kuchukuliwa ruzuku na msimamizi wake pale anapoishi,
aliishukuru serikali kupitia Tasaf kwa kumuwezesha kupata matibabu kwa urahisi
pindi alipolazwa na kununua mbuzi wawili ambao anatarajia wazae ili awauze siku
zijazo.
“Pia natumia ruzuku nazopewa kwenye kilimo hasa kwenye
manunuzi ya mbegu na mbolea na mavuno ndo kama unavyoyaona hapo, alisema Bi
Kingu huku akielekeza kidole kwenye viroba vikubwa vilivyojaa maharagwe
yaliyovunwa.
Bi Nzitu Shilla ni miongoni mwa wanufaikaji hao wa mfuko
wa Tasaf Wilaya ya Mkalama ambapo alikiri jambo kubwa alilofanya kupitia ruzuku
aliyokuwa akipewa ni ujenzi wa nyumba anayoishi ambapo alifanikiwa kununua
mabati na kufyatua matofali ya udongo imara ili kuwa na uhakika wa kutopata
madhara kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa msimu wa upepo mkali na
Mvua.
Tasaf Mkalama ilizidi kuchanja mbuga ili kujionea kwa
macho yao wenyewe matumizi ya ruzuku ambazo wamekuwa wakitoa ambapo safari hii
walibisha hodi nyumbani kwa Bertha Kingu ambaye kabla ya kuanza kupata ruzuku
alikuwa akiishi katika nyumba za watu kutokana na nyumba yake ya awali kuanguka
baada ya kutokuwa imara.
“Nilipata manyanyaso sana kutoka kwa wenye nyumba hali
ambayo kuna muda ilinilazimu nikose mpaka hamu ya kula kwani muda wote nilikuwa
nawaza nyumba ya kuhamia mara baada ya kufukuzwa lakini nashukuru nilipoingizwa
kwenye huu mpango wa ruzuku wa Tasaf nimefanikiwa kujenga nyumba yangu,ninafuga
kuku na nimefanikiwa kulima mahindi na kupata mavuno ya kunitosha” Alisema
Bertha.
No comments:
Post a Comment