Friday, 2 March 2018

DARAJA HILI LITATUTANGAZA MKALAMA

Meneja wa Wakala wa barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Ephraim Kalunde (kushoto) mapema leo  akimuongoza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. mhandisi Jackson Masaka (wa pili kutoka kushoto) na viongozi wengine waandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kukagua daraja bora na la kisasa lililojengwa katika kijiji cha Msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka (mwenye suti nyeusi) akiwa katika picha ya pamoja  na viongozi wengine waandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mapema leo muda mfupi kabla ya kukabidhiwa daraja la kisasa lililopo katika kijiji cha Msingi.

Meneja wa wakala wa barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Ephraim Kalunde akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa daraja la Msingi mapema leo.

Huu ndio muonekano wa daraja hilo baada ya kukamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga akitoa maelezo ya awali muda mfupi kabla ya hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mapema leo katika kijiji cha Msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka akimpongeza Mkurugenzi wa Kampuni ya Sindai Nicholaus Maro ambayo ndiyo iliyojenga daraja la kisasa katika kijijicha Msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka akitoa hotuba muda mfupi kabla ya kukabidhiwa daraja la kisasa la Msingi lililopo katika kijiji cha Msingi mapema leo.

Takribani shilingi Bilioni moja zimeokolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kushirikiana na Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) baada ya kukamilisha daraja la kisasa kabisa la waenda kwa miguu na vyombo vingine vya usafiri lililopo katika kijiji cha Msingi kwa kiasi cha Shilingi milioni 300,007,920.00

Usanifu uliofanywa awali na makisio ya gharama za ujenzi wa daraja hilo kwa kutumia teknolojia iliyozoeleka ya zege na nondo unaonesha daraja hilo lilipaswa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 1,300,000,000.00 lakini baada ya kubaini uwepo wa rasilimali za kutosha za mawe na mchanga, Halmashauri iliamua kujenga daraja hilo kwa kutumia rasilimali hizo tu jambo lililoifanya Mkalama kuwa ya pili kuwa na daraja la aina hiyo baada ya lile lililopo Wilayani Ludewa.

Daraja hilo lililojengwa kwa teknolojia ya Mawe na Mchanga tu lina urefu wa mita 45 huku likiwa na matundu makubwa manne ya kupitishia maji na lina uwezo wa kupitisha mzigo usiozidi tani 10.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi daraja hilo kwa wananchi wa Kata ya Msingi na wanufaika wengine wa daraja hilo ambao kwa pamoja waliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka, meneja wa TARURA wilayani hapa Mhandisi Ephraim Kalunde alisema kuwa mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ulijumuisha pia kazi ya ufunguaji wa barabara yenye urefu wa mita 605 kwa ajili ya mapokeo ya daraja.

“Mhe. Mkuu wa Wilaya, TARURA ambao ndio wasanifu na wasimamizi wa mradi huu wameweza kutumia na kuitambulisha teknolojia ya ujenzi wa madaraja na miundombinu ya barabara kwa kutumia Mawe ambayo mbali na kuwa imara zaidi, teknolojia hii ni nafuu ukilinganisha na teknolojia nyingine kama ile ya kutumia zege na nondo nyingi” Aliongeza Mhandisi Kalunde.

Mara baada ya kukabidhiwa daraja hilo kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ameipongeza timu yote iliyofanikisha kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo huku akiwataka wananchi kutunza na kulinda mradi huo kwa kutokata miti iliyopo kwenye mto unaopita chini ya daraja na kutochimba mchanga karibu na daraja hilo.

“Mbali na kuwa kivuko kwa watembea kwa miguu na vyombo vya usafiri, daraja hili ni kivutio kikubwa sana cha wageni mbalimbali waliopo nje ya Mkalama na kuna watu wengi sana kutoka sehemu mbalimbali watakuja kuona na kujifunza teknolojia hii mpya ya viwango vya hali ya juu kabisa” Alisema Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka pia aliwataka wananchi wanaoishi kando ya daraja hilo kutumia fursa ya uwepo wa kivuko hicho kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara ili daraja hilo liwe na tija ya kusafirisha mazao hayo badala ya kulitumia kupigia picha tu.

“Daraja hili ni muendelezo wa mambo mazuri yanayoendelea kufanywa na serikali ndani ya Wilaya ya Mkalama na muda si mrefu sana barabara ya kutoka Bariadi mkoani Simiyu mpaka Iguguno Mkoani Singida kupitia daraja la Sibiti itajengwa kwa kiwango cha lami na tayari serikali imeanza kutafuta fedha za kutekelezea mradi huo hivyo ndani ya kipindi cha miaka hii mitano, Mkalama itakuwa na Maendeleo makubwa sana.


Ujenzi wa daraja hilo umetumia muda wa Miezi 7 mpaka kukamilika kwake ikiwa ni nyongeza ya mwezi mmoja zaidi baada ya kuwepo kwa kazi za nyongeza ambazo hazikuwepo kwenye usanifu wa awali ambapo ulianza tarehe 07/07/2017 na umekamilika tarehe 16/02/2018.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA