Wednesday 15 November 2017

BARAZA LA MADIWANI MKALAMA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega akifungua kikao cha  baraza la Madiwani mapema leo

Waheshimiwa madiwani na Wakuu wa Idara wakiwa katika kikao cha baraza la Madiwani mapema leo

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akizungumza machache wakati wa kikao cha baraza la madiwani mapema leo



Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama limefanyika leo huku hoja mbalimbali zikiibuliwa na kupatiwa majibu.

Baraza hilo ambalo ni la kwanza kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 liliipa kipaumbele sekta ya Elimu na Kilimo ambapo madiwani walielezea hali ya utekelezaji katika sekta hizo na changamoto zinazopatikana  kutoka kwenye kata zao huku pia wakiainisha mikakati mbalimbali waliyojiwekea kukabiliana na changamoto hizo.

Moja ya hoja zilizoibuliwa katika baraza la leo ni changamoto zilizojitokeza katika zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa ambapo katika baadhi ya vijiji mashine zimeshindwa kusoma alama za vidole za baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha.

Akijibu juu ya hoja hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Godfrey Sanga amekiri kupokea taarifa za kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amewatoa hofu wananchi hao kwa sababu mamlaka husika  inaendelea kushughulikia suala hilo na pindi likipatiwa ufumbuzi wananchi hao wataarifiwa.

Diwani wa Kata ya Ilunda Mhe. Mohamedi Imbele alitaka kujua mipango na mikakati ambayo Halmashauri imeweka ili kuhakikisha kunakuwepo na maadhimisho ya Wilaya ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji  maarufu kama Nane Nane ambapo Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Mhe. Erasto Linza alimhakikishia Mhe. Imbele na Wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuwa mipango ya kuhakikisha sikukuu hiyo inaadhimishwa ngazi ya Wilaya inaendelea vizuri na hatua iliyobaki ni kupanga Sehemu ambayo maadhimisho hayo yatafanyika kwa Mwaka ujao.

Suala la utunzaji wa vyanzo vya maji lilikuwa ni moja ya mambo yaliyoibuliwa katika baraza hilo ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega alitoa msimamo wa Halmashauri ya Wilaya kuwa kuanzia sasa gharama za kurejesha huduma ya maji katika  kijiji ambacho watu wake watahujumu vyanzo na miundombinu ya Maji zitatolewa na kijiji husika na si halmashauri.

Baraza hilo hutanguliwa na baraza la Kata ambapo waheshimiwa madiwani hupokea majibu ya wataalam kuhusu changamoto mbalimbali zilizopo kwenye kata zao na kuziwasilisha kwa wataalam kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.



No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA