Mkadiriaji wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Paskazia Tibalinda akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa bweni na bwalo la Shule ya Msingi Munguli unaoendelea katika kitongoji cha Munguli |
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni chombo kilichosaidia
kwa kiasi kikubwa sana kukuza na kuboresha kiwango cha Elimu nchini kwa
kuwezesha miundombinu inayozunguka sekta hiyo nyeti kabisa Ulimwenguni hivi sasa.
Katika Wilaya ya Mkalama, Mamlaka hiyo imewezesha
kupatikana kwa miradi mikubwa miwili ambayo kwa namna moja au nyingine
itasaidia kuinua kiwango cha udahili na ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari.
Kitongoji cha Munguli ni eneo linapoishi kabila maarufu
sana la Wahdzabe ambalo kwa miaka mingi tangu kupatikana kwa Uhuru limekuwa na
mwitikio mdogo linapokuja suala la elimu hasa kutokana na kabila hilo kuishi
mbali sana na mahali zinapopatikana huduma za kijamii.
Baada ya kuona changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama kwa kushirikiana na TEA wameanza Ujenzi wa bweni na bwalo la chakula la
kisasa kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Munguli mradi ambao ukikamilika utaongeza hamasa kwa jamii hiyo kushiriki
katika haki yao ya Msingi ya kupata Elimu kwa kusaidia wanafunzi hao kuondokana
na changamoto ya kutembea umbali mrefu mpaka kufika shuleni na pia
itawahakikishia kupata huduma bora ya chakula kwa wakati hali itakayowawezesha kupata muda mrefu zaidi wa kukaa shuleni.
Kwa mujibu wa Mkadiriaji wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama,
Bi. Paskazia Tibalinda Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 184 kwa
upande wa bweni na shilingi milioni 119 kwa upande wa bwalo na unatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.
“Zoezi la uchimbaji wa msingi limechukua muda mrefu kidogo
kutokana na uwepo wa mawe kwenye udongo wa eneo hili lakini tunashukuru
tumemaliza na sasa kinachofuatia na kumwaga kifusi na jamvi ambapo baada ya
hapo kazi hii itaanza kwenda kwa kasi” Aliongeza Bi. Tibalinda.
Akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Elimu Tanzania wakati
wa ziara ya ukaguzi wa mrad huo, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi. Sylvia
Lupembe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa usimamizi mzuri wa
mradi huo ambapo ametoa rai ya kukamilika kwa mradi huo kwa wakati na katika
ubora ulioanza nao.
“Mradi huu ni maalum kwa sababu utaisaidia jamii maalum ya
Watanzania kabila la wahadzabe lakini
pia utaibadilisha jamii hii kama ambavyo wenyewe wamesema kuwa wamekaa sana
porini lakini hawatoacha Mila yao ila wanahitaji kupata elimu” Aliongeza Bi.
Lupembe.
Bi. Lupembe ameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa chachu ya kuchochea maendeleo ya Elimu kwa
kuongeza idadi ya udahili na ufaulu wa wanafunzi wa shule hiyo ambapo
alisisitiza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mpaka
kukamilika kwa mradi huo.
“TEA tumefarijika sana kusikia Halmashauri imeshaanza
kununua vitanda kwa ajili ya wanafunzi watakaoishi kwenye bweni hili pamoja na
jengo kuwa katika hatua ya awali kabisa” Alimalizia Bi. Lupembe.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
Afisa Elimu wa Wilaya ya Mkalama kwa upande wa shule za Msingi, Chacha Kehogo alisema
kuwa halmashauri imejipanga vizuri kuupokea mradi huo mara utakapokamilika
ambapo mpaka sasa tayari imeshanunua vitanda 31 ambavyo vimeshafika katika
shule hiyo vikisubiri kukamilika kwa bweni.
“ Kwa hiyo niwahakikisheni TEA kuwa halmashauri ya Wilaya
ya Mkalama itaendelea kuunga mkono jitihada mlizozionesha ili na sisi tuoneshe
tunachoweza kufanya na hata wadau
wengine wakitaka kuja wasituone tegemezi hivyo niwashukuru sana na naomba msisite
kututembelea tena kwa sababu bado tuna changamoto nyingi sana katka shule zetu
hasa upande wa miundombinu. ” Alimalizia Kehogo
Mbali na mradi huo TEA imekamilisha ujenzi wa nyumba bora
kabisa na ya kisasa ya walimu iliyopo katika kijiji cha Isanzu yenye thamani ya
shilingi milioni 148 ambapo jumla ya
Walimu tisa wa shule ya Sekondari ya Isanzu wanatarajia kuanza kuishi hapo muda
wowote kuanzia sasa.
Ili uweze kumsikia na kumuona Meneja mahusiano wa TEA Bi. Sylvia Lupembe akizungumza katika ziara hiyo tafadhali bofya hapa
Ili uweze kumsikia na kumuona Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Chacha Kehogo akizungumza katika ziara hiyo tafadhali bofya hapa
Ili uweze kumsikia na kumuona Mkadiriaji Majengo wa Halmshauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Paskazia Tibalinda akizungumza katika ziara hiyo tafadhali bofya hapa
No comments:
Post a Comment