Thursday, 14 September 2017

Ni lazima viongozi muwe na fikra na uongozi wa kimkakati-Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akizungumza na wajumbe wa Umoja wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida mapema leo asubuhi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka akijitambulisha mbele ya wajumbe wa Umoja wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida mapema leo asubuhi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega akizungumza na mbele ya Mgeni rasmi na wajumbe wa umoja huo mapema leo asubuhi.Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Daktari Rehema Nchimbi amelaani kitendo cha Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi na watu wasiofahamika akiwa kwenye gari yake kilichotokea hivi karibuni akiwa kwenye gari nyumbani kwake Dodoma.

Mhe. Nchimbi amelaani tukio hilo muda mchache kabla ya kufungua  kikao cha  Umoja wa mamlaka ya serikali za mitaa (ALAT) ngazi ya Mkoa wa Singida huku ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza hadharani kuhusiana na tukio hilo tangu kutokea kwake.

“Bila kujali itikadi za kisiasa, dini au kabila, suala lililomtokea Mhe. Tundu Lissu linapaswa kulaaniwa na kila Mtu hasa sisi wa Mkoa wa Singida kwa sababu ni Mbunge anayeutumikia Mkoa wetu na ni mwananchi mwenzetu wa Mkoa wa Singida” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi amesema kuwa ni vizuri Wananchi wote wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla wawe na subira na Imani dhidi ya vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo bado vinaendelea kulifuatilia na kuchunguza  tukio hilo kwa ukaribu.

“Si jambo jema kumnyooshea kidole mtu, kundi la watu au taasisi fulani kuhusiana na tukio hili kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo makini sana na baada ya kumaliza kazi yao vitatoa majibu sahihi yaliyotokana na uchunguzi wao hivyo kwa sasa tuwe na subira na tuungane kumuombea ndugu yetu Mhe. Lissu aweze kupona na kurejea katika majukumu yake ya kuwahudumia Watanzania” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.

Katika kikao hicho Mhe. Nchimbi amewataka viongozi wote wa halmashauri za Mkoa wa Singida kuwa na fikra  na uongozi wa kimkakati ili kuhakikisha wanawahudumia wananchi wote kutokana na rasilimali zilizopo bila kujali zinatosha au la.

“Kama utakuwa na ‘strategic thinking’ maana yake utakuwa na uwezo wa kujua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wako kulingana na rasilimali ulionazo na kamwe huwezi kuwa na kisingizio kuwa miundombinu haijitoshelezi” Alisema Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi amesema baada ya kuwa na fikra za kimkakati ni lazima viongozi wote wa Wilya husika wawe na uongozi wa kimkakati ambao utampa nafasi kila kiongozi kwa nafasi yake kutoa mchango wake katika kutatua changamoto za wananchi.

“Sio unaenda Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya na kumueleza tatizo lako anasema mimi ni ‘DC’ kwa hiyo kama ni ‘DC’  ‘so what’, ni lazima katika kila changamoto ya mwananchi mchango wa kila kiongozi uonekane” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi alihitimisha hotuba yake fupi kwa kuwataka viongozi wanaounda umoja huo Mkoani Singida kuhakikisha wanaifanya Singida kuwa Mkoa wa Viwanda kwa kuwavuta wawekezaji wengi zaidi kuchangamkia fursa nyingi zilizopo Mkoani hapa.


“Kuna ngozi nyingi sana inatoka mkoani Singida, hebu jaribuni kuangalia namna gani tunaweza kuanzisha kiwanda cha ngozi hapa na pia naomba nyie mshiriki katika Kilimo cha mazao mbalimbali yanayostawi vizuri Mkoani Singida huku mkisisitiza na wananchi nao kufanya hivyo na hatimaye tuongeze uzalishaji wa mazao yanayoupa sifa kubwa mkoa wa Singida” Alimalizia Mhe. Nchimbi.

Muangalie Mhe. Nchimbi akizungumza wakati wa kikao cha leo kwa kubonyeza hapa

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA