Thursday 6 July 2017

Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 wilayani Mkalama

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama  Mhe: Mhandisi Jakcson Masaka akizungumza machache mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ndugu Amour H.Amour muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Mkalama Mhe:Allan Kiula wakionesha ishara ya ukakamavu muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha Tumuli

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ndugu Amour H. Amour akisoma ujumbe uliowekwa  katika mradi wa Ujenzi wa bweni, bwalo la chakula na choo katika shule ya sekondari Iguguno.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ndugu Amour H. Amour akizungumza na wananchi mara baada ya kuanza kwa mbio za Mwenge Wilayani Mkalama.

Siku ya jumatatu ya wiki hii (Julai 3,2017) Wilaya ya Mkalama ilikimbiza Mwenge wa Uhuru baada ya kuupokea kutoka Wilaya ya Iramba ambapo ulikimbizwa katika Miradi 7  iliyopo Wilayani hapa huku  minne ikiwa ni ya kuwekwa jiwe la msingi, miwili ya kuzinduliwa na mmoja wa kukaguliwa/kuonwa.

Miradi hiyo ni pamoja na  wa ujenzi wa bweni kubwa la wanafunzi, bwalo la chakula na vyoo unaoendelea katika shule ya sekondari Iguguno, mradi wa maji safi uliopo katika kijiji cha Mnolo, Mradi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti na ufugaji wa nyuki uliopo katika kijiji cha Kinyangiri, mradi wa Ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa Mikutano na hadhara mbalimbali uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya katika kijiji cha Nduguti, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kijiji cha Mwando mpaka kijiji cha Nkalakala  na mradi wa soko la Vitunguu uliopo katika kijiji cha Dominiki.

Jumla ya gharama ya miradi yote hiyo mpaka kukamilika kwake ni shilingi 5,197,865,111 ambapo michango iliyotolewa kupitia nguvu za wananchi  ni shilingi 35,770,000 huku fedha iliyotolewa na serikali kuu ikiwa ni shilingi 1,694,878,769  Upande wa Halmashauri ya Wilaya imetoa  shilingi  9,580,000 huku wahisani wakitoa shilingi 467,045,111.

Katika miradi yote hiyo Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndugu Amour H. Amour amesisitiza juu ya matumizi bora ya fedha za serikali ambapo aliagiza miradi yote ilingane na thamani ya pesa iliyotumika kuikamilisha.

“Niwapongeze sana kwa kuwa na jengo zuri na kisasa kuliko yote katika Maeneo ambayo Mwenge umeshapita na naomba nisisitize juu ya utoaji huduma bora zenye kufuata weledi  kwa wananchi ili thamani na uzuri wa jengo hili uendane na huduma wanazopata wananchi huku mkizingatia kuwa madaraka mliyonayo yanatokana na uwepo wa wananchi hawa” Aliongeza Amour.

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa bweni, bwalo na vyoo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 400,  katika shule ya Iguguno Amour alisifu jitihada zilizofanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kupitia uongozi wa Shule hiyo kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo pekee yenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Wilaya ya Mkalama wanakuwa na mazingira mazuri kuanzia sehemu ya kula mpaka kulala ambapo aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

Mara baada ya kumaliza mbio zake katika Wilaya ya Mkalama, Mwenge wa Uhuru ulikabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu makabidhiano yaliyofanyika katika kijiji cha Bukundi wilayani Meatu siku ya Jumanne Julai 4, 2017.

Mwenge wa Uhuru  kwa Mwaka 2017 umebeba ujumbe unaosema “Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”




No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA