Friday 21 October 2016

DC-MKALAMA AMALIZA MGOGORO WA ARDHI

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika kata ya Ibaga mapema jana.


Kaimu katibu tawala wa Wilaya ya Mkalama ndugu Pantaleo Molel akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya azungumze na wajumbe.

Sehemu ya wajumbe wa baraza la ardhi la  kata ya Mpambala wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (hayupo pichani) mapema jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka akizungumza na wajumbe wa baraza la ardhi la kata ya Mpambala kabla ya kufanya uamuzi wa mgogoro wa ardhi ulidumu kwa muda mrefu baina ya wakazi wa eneo hilo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Chemchem akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka (katikati) orodha na aina ya vitabu vinavyopatikana katika maktaba ya shule hiyo.



Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka akikagua vitabu vinavyopatikana katika maktaba ya shule ya sekondari Chemchem.

Wanafunzi wa kidato cha nne wakimsikiliza kwa umakini Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (hayupo pichani)  alipoingia darasani kwao kwa ajili ya kuwasalimu.

Wanafunzi wa Shule ya sekondari Chemchem wakimuonesha Mkuu wa Wilaya  Mkalama namna ya kutambua aina ya chakula kupitia majaribio ya somo la biolojia. 


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka amefanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu baina ya ndugu wawili wa familia moja, Mathayo Jonathan na Abel Jonathan  wakazi wa kijiji cha Mpambala.

Katika uamuzi wake, Mhe: Masaka aliwataka ndugu hao kuheshimu sheria na taratibu za nchi na waache kusumbua wajumbe wa baraza la ardhi la kata na viongozi mbalimbali wa Wilaya na Mkoa kwa sababu tayari eneo wanalogombania lilishatolewa maamuzi ya kumilikishwa kwa watu wengine.

“haiwezekani tena  shauri hilo kujadiliwa katika ngazi ya baraza la ardhi la kata kwa sababu tayari eneo mnalogombania limeshatolewa hukumu na baraza la ardhi la Wilaya na limeshahalishiwa umiliki wake kwa watu wengine” alisema Masaka.

Masaka alimuagiza katibu tawala wa Wilaya kuhakikisha Abel Jonathan anamtafutia eneo jingine ndugu yake na suala hilo liwe limeisha rasmi.

Wakazi hao walifikisha mgogoro wao katika baraza la Ardhi la Kata ambalo lilisitisha usikilizaji wa suala hilo kutokana na eneo wanalogombania kuwa na kesi nyingine ya Msingi katika baraza la Ardhi la Wilaya ya Kiomboi.

Kesi hiyo ya baraza la Ardhi la Wilaya ilifunguliwa na  wananchi  ambao walidai kununua eneo hilo kutoka kwa Abel Jonathan  baada ya Abel kupinga kuwauzia eneo hilo.

Uamuzi wa baraza la Ardhi la Wilaya ndio ulioanzisha mvutano baina ya ndugu hao wa familia moja kwani kabla ya kuuza eneo hilo, Abel Jonathan alikuwa ameshamuuzia ndugu yake  Mathayo Jonathan ambaye anaishi Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora.

Kufuatia hukumu ya kuhalalisha umiliki wa eneo lile kwa wale wananchi, Baraza la ardhi la Kata liliamuru Abel Jonathan amtafutie ndugu yake eneo la kufidia kwa sababu halina mamlaka ya kupinga hukumu ya baraza la Ardhi la Wilaya.

Mhe: Masaka pia alitumia fursa hiyo kukagua shule za Msingi na Sekondari za Chemchem ambapo aliupongeza uongozi wa shule ya sekondari ya Chemchem kwa kuwa na maktaba yenye vitabu vinavyoendana na mtaala uliopo.

“Kuna shule ya binafsi niliwahi kuitembelea (jina linahifadhiwa), vitabu vyake vyote ni “outdated” (muda wake wa kutumika umeisha) na kila kitabu nachoulizia naambiwa hakipo” Aliongezea Masaka.

Alitoa Rai kwa wazazi na walezi wote Wilayani Mkalama kuhakikisha ubora wa shule wanazopeleka watoto wao badala ya kujiridhisha na ubora wa elimu inayotolewa kwa kuzingatia ukubwa wa ada za shule wanazolipa.



No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA