Wednesday, 13 April 2016

MKALAMA IMETEKELEZA


Baada ya jitihada mbalimbali za Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na wananchi wa Mkalama  kuhakikisha wanafunzi wote wa Wilaya ya Mkalama wanakaa kwenye madawati, hatimaye lengo la jitihada hizo limeanza kutimia baada ya madawati mia moja kukabidhiwa na kuanza kutumika katika shule ya msingi Gumanga iliyopo Wilayani hapa.

Akizungumza wakati wa kukagua madarasa ili kuhakikisha kama wanafunzi wote wamekaa kwenye madawati hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mheshimiwa Christopher Ngubiagai alisema kuwa amefarijika sana kuona tatizo la wanafunzi kukaa chini au juu ya mawe likiisha katika Wilaya yake.

“Nawapongeza sana wananchi wa Gumanga kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kutengeneza madawati 150 ikiwa ni Zaidi ya mahitaji halisi ambayo ni 104” Alisema Ngubiagai.
Ngubiagai aliongeza kuwa mpaka kufika mwisho wa mwezi huu, atahakikisha tatizo la ukosefu wa madawati linabaki kuwa historia katika Wilaya ya Mkalama ikiwa ni miezi miwili nyuma ya tarehe ya mwisho aliyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.

 “Nafurahi kwa tatizo la madawati kuelekea ukingoni kabisa katika Wilaya ya Mkalama, nataka sasa tuhamishe juhudi zetu katika kuboresha mazingira ya shule zote zilizopo wilayani kwetu”. Alisema Ngubiagai.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Ngubiagai alitumia fursa hiyo ya ukaguzi wa madawati kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Gumanga ambapo baadhi alizitolea majibu yeye mwenyewe na nyingine  zilijibiwa na kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Ndugu Chacha James Kihego.


Huu ndio muonekano wa darasa la pili katika shule ya msingi Gumanga baada ya wanafunzi kuanza kukalia madawati.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mhe: Christopher Ngubiagai (kushoto)  na Afisa Elimu wa Wilaya hiyo ndugu Chacha James Kihego wakikagua madaftari ya wanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Gumanga ili kuona tofauti iliyopatikana baada ya wanafunzi hao kuanza kukalia madawati.

Sasa Mwalimu Edith Mbuli wa Shule ya Msingi Gumanga anaweza kufundisha somo la kiswahili kwa wanafunzi darasa la pili huku akiwa na uhakika wa kueleweka  vyema baada ya wanafunzi hao kuondokana na kukaa kwenye sakafu.

Wanafunzi wakikaa kwenye madawati hata nafasi ya mwalimu kupita kukagua kazi zao inapatikana kama unavyoona wanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Gumanga baada ya kuanza kukalia madawati.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mhe: Christopher Ngubiagai ( kushoto) Afisa Elimu wa Wilaya hiyo ndugu Chacha James Kihego (katikati) na kaimu Afisa elimu Sekondari ndugu Pascal Kashaigili wakikagua madaftari ya wanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Gumanga ili kuona tofauti iliyopatikana baada ya wanafunzi hao kuanza kukalia madawati.

Huu ndio muonekano wa darasa la nne katika shule ya msingi Gumanga baada ya wanafunzi wake kuanza kukalia madawati.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mhe: Christopher Ngubiagai (kulia)  na Afisa Elimu wa Wilaya hiyo ndugu Chacha James Kihego wakikagua madaftari ya wanafunzi wa darasa la nne  Shule ya Msingi Gumanga ili kuona tofauti iliyopatikana baada ya wanafunzi hao kuanza kukalia madawati.

Wananchi wa kata ya Gumanga wakimsubiri Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai azungumze nao machache na kusikiliza kero zao.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai (katikati) akijiandaa kuzungumza na wananchi wa kata ya Gumanga.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kata ya Gumanga mambo mbalimbali yanayohusu kata yaoNo comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA