Wednesday 13 April 2016

Heko Mkuu wa Sekondari ya Jorma.


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai amefurahishwa na kumpongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari Jorma  iliyopo katika kata ya Gumanga Wilayani hapa Mwalimu  Mwanga H.B Mangi kwa kuonesha moyo wa kizalendo na kujenga bweni la kisasa kabisa kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa shule hiyo, Ngubiagai alisema kuwa mwalimu huyo anastahili kupongezwa na kupewa motisha kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa sababu kuna baadhi ya watu wakipewa pesa na serikali huzitumia kwa matumizi yao binafsi na kutekeleza miradi ya serikali chini ya kiwango au kutotekeleza kabisa.

“Kule Iramba kuna watumishi nimewasimamisha kazi na wameshafunguliwa kesi mahakamani kwa sababu walipewa milioni 133 kwa ajili ya ujenzi wa bweni tangu mwaka 2011 lakini mpaka leo bweni lile halijakamilika lakini huyu alipewa milioni 40 na amejenga bweni la kisasa kabisa tena kwa muda mfupi na bado pesa ya choo katoa kwenye bajeti yake” Alisisitiza Ngubiagai.

Aliongeza kuwa watumishi wa aina hiyo atahakikisha wanapata kila nyenzo watakazohitaji katika kutekeleza majukumu yao kwa sababu wameonesha nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kulinda rasilimali za serikali.

Kwa upande wake Mwalimu Mangi  alisema kuwa baada ya kukabidhiwa pesa hiyo, waliwasiliana na mhandisi wa Wilaya ambaye B.O.Q yake ilionesha pesa hiyo inatosha kujenga bweni la wanafunzi 48 tu ambao ni wachache ukilinganisha na uhitaji uliopo.

“Nilikaa na timu yangu tukaamua kumtafuta fundi wa hapa hapa kijijini akakiri kuwa pesa hiyo inaweza kujenga bweni zuri lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 56 ambayo ni zaidi ya idadi ya awali” Alisema Mwalimu Mangi.

Aliongeza kuwa baada ya kupata taswira hiyo, aliwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bravo Lyapembile na mhandisi wa Wilaya ambaye alisema kwa mchakato walioufanya suala hilo linawezekana hivyo wanaweza kuendelea nao na kama wakikwama wawasiliane na ofisi ya Mkurugenzi mara moja.

“Tulianza rasmi ujenzi na mafundi wetu wa hapa hapa kijijini na hatimaye jengo limekamilika na bado kuna vifaa vimebaki lakini katika pesa ile hakukuwa na bajeti ya choo hivyo niliamua kutumia bajeti yangu ya shule kujenga vyoo na ndo vipo kwenye hatua ya mwisho kukamilika”. Alimalizia mwalimu Mangi.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mheshimiwa Christopher Ngubiagai alisema atafanya kila jitihada kuhakikisha bweni jingine ambalo ujenzi wake umesimama  kutokana na kukosa fedha linakamilika na linaanza kutumiwa na wanafunzi kama ilivyokusudiwa.

“Nikifika ofisini nitaanza kufanya mchakato ili fedha zinazotakiwa kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa bweni hili zipatikane na likamilike kabla ya mwezi julai mwaka huu ili hawa watoto wetu hasa wanafunzi wa kike waondokane na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.” Alimalizia Ngubiagai.


Huu ndio muonekano kwa ndani wa bweni lililojengwa kwa pesa ya serikali na kusimamiwa  na Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Jorma.

Na huu ndo muonekano wa bweni hilo kwa nje.

Huu ndio muonekano kwa kila chumba cha bweni hilo ambapo kila chumba kina uwezo wa kuweka vitanda vinne.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA