Saturday, 14 June 2014

KUTANA NA MZEE HUYU ALIYEWAHI KUWA MLINZI WA NYERERE


Mwenge wa Uhuru ukiwa katika ziara zake za kuzunguka nchi nzima, ulipofika katika wilaya ya mkalama ulilazwa katika kijiji cha Iguguno. Moja ya mambo yaliyojiri katika mkesha huo ni kukutana na Mzee Athuman Juma wa kijiji cha Iguguno Wilayani Mkalama ambaye amewahi kuwa Mlinzi wa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere miaka ya sitini mpaka sabini. Akisimulia historia yake, Mzee huyu alieleza kuwa aliondoka kijijini kwenda Dodoma mjini kutafuta maisha akiwa Dodoma alipata nafasi ya kufanya kazi za ndani kwa Mzungu aliyekuwa akiishi Dodoma wakati huo. Jinsi alivyokutana na Baba wa Taifa alisema; akiwa kama mtumishi wa Mzungu huyu Mwl. Nyerere alikuja Dodoma kufanya mkutano na wananchi wakati akitokea katika Mkoa wa Tabora. Mzee huyu naye alifika mkutanoni ndipo alikutana na Mwl. Nyerere na mara baada ya Mwl kumwona alimwita kumwambia aingie kwenye gari na ndipo akamchukua tangu wakati huo na kwenda nate Dar es Salaam. Akiwa Dar es Salaam mzee huyu alipata mafunzo ya kijeshi wakati huo kwenye kambi mbalimbali za Dar es Salaam na wengine kama vijana wa TANU. Mzee huyu baada ya kumaliza mafunzo yake yaliyochukua miezi sita alichukuliwa Ikulu na kuwa Mlinzi wa Rais Mwl. J.K. Nyerere.
Mzee alisema kuwa wamewahi kusafiri na Mwl kwenda China, Uingereza (London), Cuba, Marekani Urusi na nchi zingine. Cha kushangaza mzee alikuwa hajui Kiingereza hivyo akiwa nje ya nchi aliongea na watanzania tu waliojua kiswahili.

Baada ya kuendelea na kazi yake kama mlinzi wa Rais mzee alipata maradhi ya tumbo ambayo yalimsababishia asiweze kuendelea na kazi yake ndipo Mwl. alimpa Tsh 700 kwenda kupata matibabu na kujiangalia hali yake nyumbani na baadae arudi kuendelea na kazi yake, lakini kwa bahati mbaya mzee huyu hakupata uwezo wa kurudi Ikulu na ndipo alipokosa mawasiliano na Mwl. na tangu wakati huo amekuwa kijijini bila msaada wowote.
Mzee huyu hakuweza kupata hata kiinua mgongo cha kazi yake kutokana na hali ya afya iliyojitokeza. Mpaka sasa mzee huyu hana msaada wowote toka serikalini na amekuwa akijishughulisha na shughuli ndogondogo ili kujikimu kimaisha.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA