Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi akianza shughuli ya kupanda viazi lishe katika shamba la kijiji cha Nkungi. |
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Jackson Masaka akipanda viazi lishe katika shamba la kijiji cha Nkungi ili kuonesha ishara kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu. |
Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Bi. Anjelina Lutambi akishiriki kwenye zoezi la upandaji wa viazi lishe katika kijiji cha Nkungi. |
Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Bi. Anjelina Lutambi akishirikiana na mwanakijiji kuchimba mashimo ya kupandia viazi lishe katika Kijiji cha Nkungi jana. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama (hawapo pichani) jana mchana. |
Watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza kwa umakini Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi alipokuwa akizungumza nao mapema jana mchana. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi au “mama
Nchimbi” kama anavyojulikana Nchini jana aliendelea na ziara yake katika Wilaya
ya Mkalama ambapo kabla ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo alishiriki katika shughuli za kilimo kwenye vijiji vya Nkungi na Ilunda.
Tukio hilo la aina yake kuwahi kufanywa na viongozi
wakuu wa serikali lilifanyika saa3 asubuhi ambapo mara tu baada ya kuzungumza
na wananchi, Mhe: Nchimbi aliamuru viongozi wote waliofika katika ziara yake
kijijini hapo akiwemo Katibu tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya Mkalama, Katibu
tawala wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama na wakuu wa idara washiriki katika
kupanda zao la viazi lishe kwenye shamba lote la wanakijiji hao.
Mhe: Nchimbi alisema lengo la kufanya zoezi hilo ni
kutoa elimu kwa wananchi kuwa jukumu la usalama wa chakula si la Wananchi au wakulima pekee bali
ni la Viongozi wote wanaowatumikia wananchi hao.
“Sipendi kiongozi anayesema yupo karibu na wananchi kwa
sababu hatuwezi kupima ukaribu uliopo hivyo ni vyema kuanzia sasa tuache kuwa
karibu na badala yake tuwe pamoja nao” Alisema Nchimbi.
Akiwa shambani hapo, Mhe: Nchimbi aliwataka viongozi
wote na watumishi wa Wilaya kulima mazao ya viazi, mihogo au kufuga nyuki ili
kuondokana na tabia ya kuilalamikia serikali kuwa mishahara inayowalipa
haitoshi.
“Mwaka huu wa Kilimo Kila Mtumishi ni lazima awe na nusu
heka ya Viazi au Mihogo au afuge nyuki mizinga miwili au afanye vyote kwa
pamoja na baada ya miezi mitatu kuanzia sasa nitapita kukagua shughuli hizo”
alisisitiza Nchimbi.
Akiwa kwenye Mkutano na watumishi wa halmashauri, Mhe:
Nchimbi aliagiza kabla ya kusaini mkataba viongozi wote wa halmashauri ni
lazima wakiri thamani ya mali zao zinazohamishika na zisizohamishika ili kama
mradi utatekelezwa chini ya kiwango, mali zao zitumike kufidia pesa ya serikali
iliyopotea.
“Mradi wakati unajengwa Mkurugenzi, Mwenyekiti wa
halmashauri na wataalam wanauangalia bila kusema chochote, ukikamilika ndio wanakuambia
umejengwa chini ya kiwango, kuanzia sasa sitaki kusikia msamiati wa ‘chini ya
kiwango’.
Mhe: Nchimbi alimalizia kwa kuwaagiza wakuu wote wa
shule za msingi na sekondari kuwaruhusu wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo
wa kushona sare za shule waendelee na masomo ili mradi taratibu nyingine wawe
wamekamilisha.
“ Baada ya Elimu kuanza kutolewa bure, changamoto
nyingine iliyobakia kwa baadhi ya wazazi ni uwezo wa kuwashonea watoto wao sare
za shule, sasa ninaagiza wakuu wa shule za sekondari na Msingi wote Wilayani
hapa kuwaruhusu watoto hao waingine madarasani hata kama hawajavaa sare za
shule ili wasikose haki yao ya msingi kwa sababu ya sare tu”. Alimalizia
Nchimbi.
No comments:
Post a Comment