Sunday 24 April 2016

ELIMU IENDANE NA UJUZI- NGUBIAGAI



Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambaye pia ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Christopher Ngubiagai akiteta jambo na Mkuu wa shule ya Sekondari Tumaini Bi Honoratha Mbiaji wakati wa sherehe za mahafali ya tisa ya kidato cha sita yaliyofanyika jana shuleni hapo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tumaini bi Honoratha Mbiaji akisoma taarifa ya shule wakati wa sherehe za mahafali mbele ya Mgeni Rasmi wa mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya  Mkalama na kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe:Christopher Ngubiagai.

Mgeni rasmi wa Mahafali ya tisa ya Shule ya sekondari Tumaini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama na kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba  Mhe:Christopher Ngubiagai akitoa hotuba yake katika mahafali hayo yaliyofanyika shuleni hapo jana.

Wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya Tumaini wakisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Christopher Ngubiagai wakati wa sherehe yao ya mahafali iliyofanyika jana.

Sehemu ya Waanafunzi wa Shule ya Sekondari Tumaini wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi wa mahafali iliyofanyika shuleni kwao jana, Mhe: Christopher Ngubiagai.



Wazazi na Walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari Tumaini wakimsikiliza Mgeni rasmi wa mahafali yaliyofanyika jana shuleni hapo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai.


Mgeni rasmi wa mahafali ya tisa ya kidato cha sita katika shule ya sekondari  Tumaini mwishoni mwa sherehe alipata nafasi ya kupiga picha na viongozi mbalimbali wa shule hiyo, Tarafa, Wilaya ya Iramba na wanafunzi wa kidato cha sita wote.




Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai amewataka wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita kujiongezea ujuzi zaidi ili kukabiliana na hali ya upungufu wa ajira iliyopo hii sasa.

Ngubiagai aliyasema hayo katika mahafali ya tisa ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Wasichana ya Tumaini iliyopo katika Wilaya ya Iramba ambako alikuwa mgeni rasmi wa mahafali hayo.

“Hakuna nchi yoyote duniani ambayo imefanikiwa kutoa nafasi za ajira kwa raia wake wote hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha mbali na elimu kubwa mnayopewa shuleni na mtakayoipata mkienda vyuo vikuu, mnakuwa na ujuzi wa ziada katika fani mbalimbali” Alisema Ngubiagai.

Aliongeza kuwa ni vizuri wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kuhakikisha wanasomea fani zenye soko kubwa la ajira ili kuepuka kuzunguka muda mrefu kutafuta ajira.

“Nawashauri wakati mnajiunga na vyuo mkasomee fani ya ualimu kwa sababu ni fani yenye heshima kubwa  na kila mtu mnayemuona amefanikiwa hii leo alipitia mikononi mwa mwalimu” Alisisitiza Ngubiagai.

Katika hatua nyingine Ngubiagai alisema kuwa ni lazima jamii ishiriki katika maendeleo ya Elimu katika maeneo waliyopo badala ya kuiachia serikali kila kitu.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dokta John Pombe Magufuli kwa mapenzi aliyonayo dhidi ya elimu ya Tanzania amefuta karo kuanzia ngazi ya Elimu ya Msingi hadi sekondari, tumuunge mkono kwa kukarabati miundombinu ya shule zetu pale tunapoona haijakaa sawa” Aliongeza Ngubiagai.

Alisema ni vizuri kwa wazazi na walezi kushiriki kuchangia ukarabati wa miundombinu ya shule badala ya kuchangia kwenye sherehe na hafla peke yake. 

“Wazazi na walezi ni lazima mbadilike, sio tu muwe mbele kutunza kwenye “kitchen party” na siku hizi nasikia zipo za wanaume zinaitwa “beg party”. Tusisubiri serikali kuja kukarabati mindombinu ya elimu  katika maeneo ambayo ni watoto wetu wenyewe ndio wanaoathirika na hali hiyo”. Alimalizia Ngubiagai.

KUSIKILIZA HOTUBA YOTE ALIYOITOA MKUU WA WILAYA YA MKALAMA MHESHIMIWA CHRISTOPHER NGUBIAGAI   bonyeza hapa




No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA