Wednesday, 14 March 2018

MKALAMA IMEPOKEA VIFAA TIBA VYA MIL. 345,430,700

Kontena lililosheheni vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 345,430,700. likipakuliwa vifaa hivyo katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama tayari kukabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Mhandisi Jackson Masaka.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama akiwaongoza viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za Wilayani  hiyo kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 345,430,700 mapema leo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama akizungumza machache muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya hiyo wakati wa hafla fupi ya kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 345,430,700.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Daktari Deogratias Masini (mwenye koti la suti) akimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya hiyo Mhe. Mhandisi Jackson Masaka namna kitanda cha wagonjwa kinavyoweza kuwa katika mitindo tofauti mapema leo katika hafla fupi ya kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 345,430,700.

PICHA 3 CHINI: SEHEMU YA VIFAA TIBA VILIVYOKABIDHIWA LEO.

Hamashauri ya Wilaya ya Mkalama leo imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya baada ya kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 345,430,700.00 kutoka taasisi ya HumanBridge yenye makao yake makuu nchini Sweden.

Miongoni mwa Vifaa hivyo ambavyo kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mkalama vilikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Jackson Masaka vinajumuisha Meza kwa ajili ya Upasuaji, Vifaa vya upasuaji, Magodoro 25, Vitanda 25, Mashine ya kupima mapigo ya moyo, Vitanda vya kujifungulia kwa wajawazito, Viti vya walemavu wa miguu, vifaa vya kusaidia kutembea kwa wanaosumbuliwa na miguu na vingine vingi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mgeni rasmi wa hafla hiyo ya mapokezi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliishukuru taasisi hiyo hiyo kwa kuichagua Mkalama kuwa Wilaya ya kwanza kupokea msaada wa aina hiyo ambapo aliwashukuru pia kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada zake za kuboresha sekta ya afya nchini.

“Alipoingia tu madarakani, Mhe. Rais Magufuli alianza na sekta ya afya ambapo aliongeza wodi kwa ajili ya wanawake pale katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo kitendo hiki ni ishara pekee ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais” Alisema Mhe. Masaka.

Mhe. Masaka aliiomba taasisi hiyo kuendeleza ushirikiano waliuoanzisha na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo aliwaahidi kutunza na kusimamia matumizi ya vifaa tiba hivyo ili kuhakikisha wananchi wa Mkalama wanafaidika ipasavyo na uwepo wa vifaa hivyo katika zahanati na vituo vyao vya Afya pindi wakienda kutibiwa.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga mbali na kuishukuru taasisi hiyo, alisema kuwa vifaa hivyo vitamaliza mapungufu ya vifaa tiba yaliyokuwepo katika zahanati na vituo vya Afya vilivyopo Wilayani hapa.

“Hata hii thamani ya vifaa iliyotajwa ni kwa mujibu wa vile ambavyo vipo kwenye rejesta ya Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD)  lakini kuna vifaa vingine vingi ambavyo tumeletewa hatujajua thamani yake kwa sababu havipo kwenye rejesta ya MSD hivyo thamani ya vifaa tulivyokabidhiwa vinaweza kufika mpaka milioni 400” Alisema Sanga.

Sanga aliongeza kuwa vifaa hivyo vimefika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika wakati sahihi kwa sababu tayari Halmashauri hiyo mbali na kuendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyambuli hivi sasa, halmashauri hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga kiasi cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya uboreshaji wa kituo cha Afya cha Mkalama, Shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wa kituo cha Afya cha Kinyangiri na shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo cha Afya cha Msiu.

Kwa upande wake muwakilishi wa taasisi ya HumanBridge Mchungaji Bahati Kito alisema kuwa jitihada zilizooneshwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kuhakikisha vifaa hivyo vinatoka bandarini haraka na kufika kwa walengwa zinapaswa kuigwa na Halmashauri nyingine kwani zimezidi kuwashawishi kutoa misaada mingine zaidi.

“Moja ya Vitu ambavyo viliikatisha tamaa taasisi yetu kutoa misaada mbalimbali nchini Tanzaniani suala la urasimu hasa baada ya mizigo yetu kufika bandarini ambapo baadhi ya makontena tuliyotuma yaliishia kuozea bandarini” Aliongeza Mchungaji Kito.

Mchungaji Kito alimalizia kwa kupongeza juhudi za dhati zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  katika kulinda rasilimali za Watanzania jambo ambalo linawapa moyo sana washirika wa nchi waliopo nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA