Saturday 28 May 2016

WAHADZABE WAKUBALI MAENEO YAO KUPIMWA

  
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na ujumbe wa wahadzabe uliofika ofisini kwake mapema jana.

Ujumbe wa jamii ya wahadzabe ukimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati) alipokuwa akizungumza nao jana.

Mwenyekiti wa jamii ya wahadzabe Edward Mashimba (mwenye suti ya blue) akiwa na wawakilishi wengine wa jamii hiyo huku wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai.


Kikao kilichofanywa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi ya Mkurugenzi wa halmshauri ya Wilaya ya Mkalama tarehe 20/05/2016 katika kata ya Munguli kuhusiana na suala la jamii ya Wahadzabe kunyang’anywa maeneo yao kimezaa matunda baada ya jamii hiyo kukubali kupimiwa maeneo yao ili waweze kuyamiliki kisheria.

Ujumbe wa wawakilishi sita wa jamii hiyo uliofika katika ofisi za Wilaya ya Mkalama na kukutana na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe: Christopher Ngubiagai, umesema kuwa wahadzabe wameamua kufanyia kazi ushauri uliotolewa na Mkuu wa Wilaya na kuungwa mkono na kaimu afisa ardhi wa Wilaya ya Mkalama Imikigwe Mwanitu kuwa maeneo yote wanayomiliki yapimwe ili wawe na umiliki wa kisheria.

Ujumbe huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe waishio Wilaya ya Mkalama ndugu Edward Mashimba umemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha hawanyang’anywi haki yao ya kumiliki maeneo ambayo wamekuwa wakiyamiliki kwa miaka mingi sasa.

Akizungumza wakati wa mazungumzo hayo ofisini kwake, Mhe: Ngubiagai aliipongeza jamii yote ya wahadzabe kwa kukubali ushauri wake na kuchukua hatua hiyo ya kukubali kupimiwa maeneo yao na kuahidi kuwasaidia kulinda rasilimali hiyo.

“kwa sababu mkishapimiwa mtakuwa mkiyamiliki maeneo hayo kisheria, ofisi yangu itahakikisha hakuna uvamizi wowote unaofanyika katika maeneo yenu na yoyote atakayevamia basi sheria itafuata mkondo wake, Alisema Ngubiagai.

Mwisho wa mazungmzo hayo mafupi, Mwenyekiti wa wahdazabe alimuombea dua ya kihadzabe Mkuu huyo wa Wilaya iliyobeba ujumbe wa kumtakia afya njema na ulinzi katika shughuli zake za kila siku za kuwahudumia wananchi.

Mbali na Mwenyekiti wa jamii ya wahadzabe, wajumbe wengine walioambatana nae ni Charles Mtani, Mathayo Wilson, Marta Marko, Pendo Daniel na Elineema Martini.


No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA