Saturday 14 May 2016

OLE WAO WANAOPOKEA RUSHWA: NGUBIAGAI

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Mng'anda.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mng'anda William Makala akisoma taarifa fupi ya shughuli mbalimbali za Maendeleo za kijiji hicho.

Afisa Tarafa wa  Nduguti Josiah Pangani akitoa maelezo machache kwa wananchi kabla ya kumkaribisha kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ili aweze kumkaribisha Mkuu wa Wilaya hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Lunzegere Kilala akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya hiyo ili aweze kuzungumza na wananchi wa Mng'anda.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mng'anda.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mng'anda wakimsikiliza  Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara yake jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Kilyungu iliyopo katika kijiji cha Mwando

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kilyungu wakimsalimia Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai na ujumbe wake mara baada ya kuwasili shuleni hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai na ujumbe wake wakikagua kazi mbalimbali za kitaaluma kwa wanafunzi wa Shule ya msingi Kilyungu.

Hii ni sehemu ya madawati yaliyotengenezwa katika Shule ya Msingi Kilyungu huku yakikaguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mwando wakiwa tayari kumsikiliza  Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara yake jana.

Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwando Jeremia Manase akimsomea taarifa fupi ya kijiji hicho Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwando katika ziara yake jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Maziliga

Mkuu wa Shule ya Msingi Maziliga David Mbugulu akimsomea Mkuu wa Wilaya ya Mkalama taarifa fupi ya shule hiyo.

Hivi ndivyo wanafunzi wa Shule ya Msingi Maziliga wanavyokaa darasani ambapo badala ya kukaa chini kama ilivyokuwa hapo awali, sasa wanakaa wanafunzi wawili katika kila dawati.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Maziliga  Athumani Makia  akisoma taarifa fupi ya shughuli mbalimbali za Maendeleo za kijiji hicho.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Maziliga  wakimsikiliza  Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara yake jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kijiji cha Maziliga katika ziara yake jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (kushoto) akiwasili katika Shule ya Msingi Nduguti katika ziara yake jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Nduguti.


Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nduguti  Nkwangu M. Nkwangu  akisoma taarifa fupi ya shughuli mbalimbali za Maendeleo za kijiji hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi waliojitokeza katika kijiji cha Nduguti ambacho ndio kilikuwa kijiji cha mwisho katika ziara yake jana.

“Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea Rushwa” Hiyo ni kauli ya kwanza kabisa iliyotolewa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kilyungu kabla ya kutoa salamu kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai aliyeambatana na ujumbe wa viongozi mbalimbali kutoka katika halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za Maendeleo kwenye Vijiji vinne vya Tarafa ya Nduguti ambavyo ni Mng’anda, Mwando, Maziliga na Nduguti.

Katika Ziara hiyo ambayo ilijuimuisha kupokea taarifa ya maendeleo ya utengenezaji wa madawati na kukagua yale yaliyotengenezwa kama yameshaanza kutumiwa na walengwa, Ngubiagai allipongeza juhudi na jitihada kubwa iliyofanywa na  Viongozi na wajumbe wa kamati za shule, Maafisa watendaji wa Vijiji, Afisa Mtendaji wa kata na Afisa tarafa wa Nduguti kwa kazi kubwa ya kukamilisha asilimia 85 ya utengenezaji wa madawati hayo.

“Baada ya kukagua kazi hii katika tarafa nyingine,  nina Imani kubwa kabisa kuwa tatizo la uhaba wa madawati katika Wilaya yangu litaisha kabla ya Juni 30 aliyoagiza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli” Alisema Ngubiagai.

Katika ziara hiyo ambayo iliambatana na mikutano ya hadhara katika kila kijiji baada ya ukaguzi wa shughuli hizo, Ngubiagai alisisitiza Wananchi wa Wilaya yake kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwani pesa hizo ndizo zinazotumika kuratibu shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Watanzania wamekuwa mabingwa sana wa kudai haki bila kutimiza wajibu jambo ambalo linaipa serikali wakati mgumu wa kutekeleza matakwa yao hivyo ni lazima wananchi muanze kwa kutimiza wajibu wenu ili serikali iwape haki zenu mnazostahili kwa sababu siku zote hakuna haki bila wajibu” Aliongeza Ngubiagai.

Katika hatua nyingine Ngubiagai alizitaka idara na watendaji  mbalimbali waliopo katika Wilaya yake kutoa huduma kwa wananchi bila upendeleo wa kisiasa, kidini, kikabila, kikanda au uwezo wa kifedha.

“Sasa hivi imefikia hatua, mtu akitaka nakala fulani ya kutoka ofisi ya serikali anaambiwa atoe pesa ya muhuri, sahihi na muda mwingine anadaiwa  pesa ya usumbufu, Mtumishi wa serikali analipwa mshahara kwa ajili ya kumtumikia mwananchi hivyo chochote kinachotolewa na Mwananchi kinyume na taratibu za serikali ni Rushwa na nitakapombaini mtumishi huyo nitamshughulikia mara moja, Alisema Ngubiagai.

Pia Ngubiagai aliwataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama kuhakikisha wananchi wanatumia pesa wanazopata kutokana na mavuno ya mazao yao kufanyia shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga nyumba za kisasa na kuondokana na nyumba za tembe zilizopo hivi sasa kwani zinahatarisha sana maisha ya wananchi hao na mali zao hasa msimu wa mvua.

“Nikiwa pale kwangu nikisikia mvua inanyesha, hofu yangu kubwa huwa inakuwa kwenu wananchi wa Mkalama na huwa najiandaa kabisa kupokea taarifa za kuanguka kwa tembe kadhaa hivyo ifike mahali tuseme inatosha kwa vifo vinavyoweza kuepukika” Alisema Ngubiagai.

Aidha Ngubiagai aliitumia ziara hiyo kwa kuwataka Wananchi wote wa Wilaya yake kuwa makini na wageni wanaoingia na kutoka ndani ya Wilaya hiyo kwani wageni wengine hawana nia njema na wananchi wake na huingia kwa lengo la kuvunja  amani na kufanya makosa ya uhalifu huku akitolea mfano wa tukio lililotokea katika Wilaya ya Sengerema hivi karibuni ambapo watu saba wa familia moja waliuawa na watu wasiojulikana.

“Kama kuna mgeni, hakikisha unampeleka kwenye ofisi ya kijiji ili akahojiwe na kufanyiwa uchunguzi zaidi na kiongozi wa kijiji akijiridhisha ndipo anaweza kurejea kwa mwenyeji wake na kuendelea na ziara yake lakini atakapotiliwa mashaka, wananchi mtoe ushirikiano kwa mgeni huyo kuondoka mara moja na kama atakamatwa na vidhibiti mbalimbali basi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake” Alimalizia Ngubiagai.
  
KAMA WEWE NI MMOJA KATI YA WALE WANAOPENDA KUKATISHA MASOMO YA WANAFUNZI WA KIKE KWA KUWAPA UJAUZITO bonyeza hapa ILI UPATE UJUMBE WAKO KUTOKA KWA MKUU WA WILAYA YA MKALAMA MHE: CHRISTOPHER NGUBIAGAI.

No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA