Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe (Kulia) akisalimiana na Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan Kiula mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana. |
Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akisalimiana na Diwani Viti Maalum wa Kata ya Iguguno Mhe. Mariam Kahola mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana. |
Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akisalimiana na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Lilian Kasanga mara baada ya kuwasili katika Mradi wa Maji wa Iguguno jana. |
Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe akifungua bomba ya maji kama ishara ya ufunguzi wa huduma ya maji katika kata ya Iguguno mapema jana |
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe
ameuhakikishia uongozi wa Wilaya ya Mkalama kuwa kufikia mwaka 2020 tatizo la
Maji litakuwa historia katika Wilaya hiyo.
Mhe. Kamwelwe ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara
yake ya Kikazi Wilayani Mkalama ambapo pamoja na mambo mengine amefurahishwa na
kasi ya maendeleo ya Wilaya hiyo huku akiwapongeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi
Mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge wa jimbo la Mkalama kwa
ushirikiano mkubwa walionao katika kuhakikisha Mkalama inapiga hatua siku zote.
“Mbunge wenu amekuwa akiniomba sana nifike huku ili
nijionee changamoto ya Maji na
nilimhakikishia kuwa ntakuja tena nashukuru nimekuja kipindi cha kiangazi ili
nijionee hali ya upatikanaji wa huduma ya maji wakati huu ambao maeneo mengi
huwa ni makavu” Alisema Mhe. Kamwelwe.
Akiunga mkono wazo la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mkalama ambaye alimuomba fedha zinazotumika kuwekea miradi ya maji zitumike
kuchimbia visima virefu badala ya kuendelea na miradi hiyo ambayo mbali na kuwa
na gharama kubwa huchukua muda mrefu kukamilika na hutoa huduma kwa watu
wachache, Mhe. Kamwelewe amesema kuwa kuanzia sasa fedha hiyo ambayo ni zaidi
ya shilingi milioni 500 kwa mwaka zitatumika
kuchimba visima hivyo ili kufikia mwaka 2020 tatizo la maji katika
Wilaya hiyo libaki kuwa historia.
“Katika kutekeleza hilo leo ntaacha visima virefu kumi ili
tuwe tumeingia kwenye vitendo moja kwa moja huku kila awamu tutakuwa tukitenga fedha ya kutosha kwa ajili
ya kumaliza tatizo la Maji Mkalama” Alisema Kamwelwe.
Akiwa katika kijiji cha Kidarafa kilichopo kata ya Mwanga
Mhe. Kamwelwe alivutiwa na maendeleo na mchango unaotolewa na kata hiyo katika
uzalishaji wa chakula na uingizaji wa
pato la Wilaya ambapo alisema kuwa mfuko wa maji wa kijiji hicho ni mdogo sana
ukilinganisha na gharama ya mafuta ya shilingi laki moja kwa siku jambo ambalo
litasababisha jumuiya ya watumia maji wa kijiji hicho kushindwa kumudu gharama
za uendeshaji wa mradi huo hivyo alimuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ampelekee gharama za
kuunga umeme wa jua ili wananchi hao
waendelee kupata huduma hiyo ya maji.
“Ninataka baada ya kuweka mitambo ya sola gharama ya maji
ishuke kutoka shilingi 50 kwa ndoo mpaka shilingi 20” Aliagiza Mhe. Kamwelwe.
Akimkaribisha Mhe.
Naibu waziri na kuwasilisha taarifa ya
hali ya huduma ya maji kwa Wilaya ya Mkalama Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe.
Mhandisi Jackson Masaka amesema kuwa mpaka sasa ni asilimia 43 pekee ya
wananchi wa Wilaya hiyo wanaopata huduma
hiyo huku vyanzo vinavyotoa huduma hiyo vikiwa ni 186 kati ya 264 huku
vyanzo 78 vikiwa havitoi huduma kutokana na sababu mbalimbali.
“Mhe. Naibu Waziri, Utekelezaji wa miradi mbalimbali
Wilayani Mkalama unahusisha wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Serikali kuu pamoja
na Benki ya Dunia” Aliongeza Mhe.
Masaka.
Mhe. Masaka alihitimisha taarifa yake kwa kutaja
changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa utoaji wa huduma ya maji Wilayani
Mkalama ambazo ni pamoja na Ukosefu wa Vitendea kazi, ufinyu wa bajeti na uchache
wa watumishi wa idara ya maji.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Allan
Kiula alimshukuru Mhe. Waziri kwa kukubali ombi lake na kufika Mkalama ambapo
alimhakikishia kuwa ataendelea kushirikina na Wizara yake bega kwa bega ili
kuhakikisha malengo ambayo Wizara imeweka juu ya Wilaya ya Mkalama yanatimia.
“Mimi ni Mwakilishi wa wananchi hivyo kila changamoto
nayopewa ni lazima niifikishe kwa watendaji na matokeo yake ndio haya na
ntajitahidi kuhakikisha kila Waziri
anayehusika na changamoto zilizopo Mkalama anafika hapa ili kujionea mwenyewe
hali halisi” Alimalizia Mhe. Kiula.
Muone Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega wakati akizungumza katika kata ya Kikonda jana kwa kubonyeza hapa
No comments:
Post a Comment