Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika banda la Wilaya ya Mkalama. |
Mapema leo jioni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema
Nchimbi ametembelea banda la halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo ametoa
maagizo mbalimbali kwa Mkurugenzi, Mwenyekiti wa Halmashauri na Afisa Kilimo wa
Wilaya kuhakikisha maonesho yanayokuja ya Nanenane yanakuwa na tija kubwa hata
kwa mwananchi wa Mkalama ambaye hajabahatika kufika katika Maonesho ya kikanda.
Mhe. Nchimbi amesema kuwa Kuanzia sasa Wilaya ya Mkalama
itenge eneo kubwa ambalo litawekwa vipando ambavyo vitakuwa hapo kwa kipindi
cha Mwaka mzima ili wananchi ambao hawatopata fursa ya kushiriki katika
maonesho ya kikanda na kitaifa watumie nafasi hiyo kwenda kujifunza kilimo bora
na cha kisasa.
“Ninaposema mwaka mzima namaanisha katika maeneo hayo
mfanye utaratibu wa kuchimba visima kwa sababu mvua haipatikani mwaka mzima na
hapo wananchi kutoka sehemu mbalimbali watafika na kupata elimu tena vipando
hivyo mnaweza kuviita ‘NaneNane Mkalama Mubashara’ mkimaanisha wananchi
watakuja kujifunza moja kwa moja kutoka
shambani” Amesisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesema kuwa kitendo hicho kitawafanya
wananchi wote wa Mkalama waone umuhimu wa sikukuu ya NaneNane kwa sababu pamoja
na kutofika katika maonesho ya kikanda na kitaifa bado watakuwa wamepata elimu
inayofanana na wale waliohudhuria maonesho hayo kikanda na kitaifa.
“Ikifika Mwezi Septemba nitafuatilia hili ili nijue kama
utekelezaji wake umeanza” Ameongeza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi pia ameagiza halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ihakikishe
imetangaza bidhaa zake kila inapotimia robo mwaka na bidhaa hizo zisiishie
kutangazwa katika redio za mikoani tu bali ununuliwe muda katika vituo vya Televisheni
pia.
“Kupitia vipindi hivyo tangazeni kila kinachozalishwa
Mkalama vikiwemo vitunguu, asali, nyanya na kwa kufanya hivyo mtakuwa
mmetangaza soko la Mkalama sio tu kitaifa bali kimataifa” Amesisitiza Mhe.
Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesifia Vitunguu vinavyozalishwa katika
Wilaya ya Mkalama ambapo amesema vina ubora wa kimataifa na hata sokoni ndio
vitunguu vinavyopewa kipaumbele kuliko vitunguu vinavyozalishwa katika maeneo
mengine.
“Kuna baba mmoja ni mstaafu wa jeshi alilima vitunguu
katika Mkoa wa Morogoro tena vitunguu vizuri tu lakini alipovipeleka sokoni alikataliwa
na kuambiwa vitunguu pekee vinavyonunuliwa hapo ni vile vinavyotoka Mkoani
Singida kwa hiyo tangazeni sana bidhaa zenu kwa sababu zina thamani kubwa sana
sokoni” Alimalizia Mhe. Nchimbi.
Ili uweze kumuona Mhe. Nchimbi akitoa maagizo hayo bofya hapa
No comments:
Post a Comment