Thursday, 15 December 2016

MKALAMA INAKABILIWA NA CHANGAMOTO NYINGI KUPAMBANA NA UKIMWI

Mratibu wa Ukimwi (W) kutoka idara ya Maendeleo ya Jamii Goodluck Mlau akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za Ukimwi kwa Wilaya ya Mkalama.


Sehemu ya Wadau wa Ukimwi Wilayani Mkalama wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa taarifa mbalimbali katika kikao cha Wadau wa Ukimwi.
Mratibu wa Ukimwi kutoka Idara ya Afya Vivian Mpangala akiwasilisha Taarifa ya hali halisi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kwa Wilaya ya Mkalama.


Sehemu ya wadau wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali kwa umakini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe: James Mkwega akizungumza machache kabla ya kufunga kikao cha wadau wa Ukimwi kwa mwaka huu.



Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo imekuwa ikitekeleza afua za ukimwi kila Mwaka hali inayosababisha kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo.

Akitoa takwimu katika kikao cha wadau wa Ukimwi kwa mwaka huu, Mratibu wa masuala yanayohusu ugonjwa huo Goodluck Mlau amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kuanzia mwezi Januari mpaka Disemba mwaka huu ni 3.01% hiyo ikimaanisha katika kila kundi la watu 100, watatu kati yao wana maambukizi ya Ukimwi.

Akizungumzia jitihada mbalimbali zilizofanywa na Idara yake katika kuhakikisha maambukizi yanashuka zaidi na kutoweka kabisa, Mlau amesema moja ya njia walizotumia ni kutoa mafunzo kwa njia ya sinema ambapo vijiji 10 vilipata huduma hiyo iliyoenda sambamba na zoezi la upimaji wa hiari, Ushauri Nasaha na ugawaji wa kondomu za kike na kiume.

“Pia siku ya Ukimwi Kiwilaya ambayo tuliadhimisha katika kijiji cha Ishenga kata ya Kinyangiri tuliandaa burudani mbalimbali za uimbaji na mchezo mmoja wa mpira wa miguu ambapo mshindi wa kwanza kwa upande wa mpira wa miguu alipewa zawadi ya seti moja ya jezi na mpira mmoja huku mshindi wa pili akipewa mpira mmoja.

Pamoja na jitihada za kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kinapungua katika Wilaya ya Mkalama, Mlau aliainisha changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili idara yake katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na Ukosefu wa usafiri wa uhakika kufuatilia masuala ya Ukimwi, Uhaba wa vituo vya kupima na kutoa ushauri nasaha (CTC), Jamii kutojitokeza kwa hiari kwenye vituo vya kutolea huduma, Fedha kidogo inayotengwa kwa ajili ya shughuli za Ukimwi na Uelewa mdogo wa jamii juu ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi na utumiaji wa kondomu.



No comments:

Post a Comment

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA