Zoezi la uhakiki wa mara ya tatu katika Mkoa wa Singida limeendelea tena leo
ambapo timu ya wahakiki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida imeanza kazi
hiyo ya uhakiki wa kujiridhisha katika Wilaya ya Mkalama.
Uhakiki huo ambao unajumuisha kada zote za watumishi wa
serikali kuu na wale wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika kwa muda wa
siku tatu kuanzia leo ambapo unatarajiwa kufikia tamati siku ya Jumatano.
Mara baada ya kufika katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya
ya Mkalama, timu hiyo ya wahakiki ilikutana na wakuu wa idara na vitengo
mbalimbali vilivyopo katika ofisi hiyo na kufanya kikao kifupi cha ufafanuzi na
maelekezo chini ya Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Njelu Abdallah.
Akizungumza katika kikao hicho, mmoja wa wahakiki hao Mbwana Mkingule alisema
wahakikiwa wote wanapaswa kuwasilisha barua za ajira, barua za kuthibitishwa
kazini na barua ya mwisho ya kupandishwa cheo kwa watumishi waliopandishwa
madaraja yao.
“Kila mkuu wa idara anapaswa kuorodhesha majina ya
watumishi wote waliopo chini ya idara yake na mwisho wa orodha hiyo kuwe na
saini za Mkuu huyo huyo wa idara na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya”
Aliongeza Mkingule
Aidha Afisa Utumishi wa Wilaya ya Mkalama, Pascal Lefi
alipendekeza watumishi wa idara ya afya kuanza kuhakikiwa kutokana na unyeti wa idara hiyo kwa
wananchi hivyo wanapaswa kuwahi kurejea kwenye vituo vyao vya kazi kuendelea
kutoa huduma.
PICHA TATU CHINI ZIKIONESHA WATUMISHI WALIOJITOKEZA KATIKA SIKU YA KWANZA YA UHAKIKI WA WATUMISHI KATIKA OFISI ZA HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA LEO MAY 9, 2016.
No comments:
Post a Comment