Akizungumza katika harambee hiyo, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, mheshimiwa Christopher Ngubiagai alisema kuwa amefarijika kwa mwitikio mkubwa aliouona siku hiyo na kuwashukuru wale wote ambao wamejitokeza na kuchangia katika harambee hiyo huku akisisitiza kuwa kampeni za aina hiyo zinapaswa kufanyika mara kwa mara.
"Mpaka sasa hatujui lini mheshimiwa Rais atafanya uteuzi au uhamisho wa wakuu wa Wilaya lakini naomba nitumie nafasi hii kuwasihi muendelee na jithada hizi za kuboresha Elimu ya Wilaya ya Mkalama hata kama mimi nitaondoka" Aliongeza Ngubiagai.
Katika hatua nyingine, Ngubiagai aliitumia siku hiyo kutoa zawadi ya baiskeli kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2015 kama sehemu ya ahadi yake aliyoitoa wiki chache zilizopita kwa wanafunzi hao.
Wanafunzi hao pamoja na shule wanazotokea kwenye mabano ni pamoja na Said Jumbe Shagodo (CHEMCHEM), Petro Stephano Mpanda (IKUNGU), Gakii Yeremia Shuba, (MNOLO), Baraka Ramadhani Hango (SOPHIA), Richard Nyahird Misobi (IKUNGU), Mwanaid Salum Pesambili (CHEMCHEM), Almasi Haruna Omary (INSHINSI), Ismail Mohamed Rajabu (MNOLO), Maria Issack Benjamen (CHEMCHEM), Juliana Steven Paulo (MNOLO), David Balanda John (MSISAI) na Agnes Aron Kishai (CHEMCHEM).
Naye Mbunge wa jimbo la Mkalama Mheshimiwa Allan Kiula mbali na kutoa kiasi cha shilingi milioni saba kutoka kwenye mfuko wa mbunge na shilingi milioni moja kutoka kwenye akiba yake binafsi alisisitiza wazazi na walezi kuwa na utamaduni wa kutembelea shule wanazosoma watoto wao ili kujionea mazingira ambayo watoto wao wanapata elimu.
"Nilijaribu kufanya utafiti na kugundua kuwa wazazi wengi hawafiki katika shule ambazo watoto wao wanasoma hivyo inakuwa ni vigumu sana kujua changamoto wanazopata walimu na wanafunzi katika shule walizopeleka watoto hao".
Akifunga harambee hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ndugu James Nkwega mbali na kuwashukuru wote waliojitokeza na kuchangia katika harambee hiyo, alimuomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli kutomuondoa Mkuu wa Wilaya hiyo kwa sababu amekuwa kiungo kikubwa sana cha kuchochea maendeleo katika Wilaya hiyo tangu alipoanza kazi mwezi Oktoba mwaka jana.
"Nitumie fursa hii pia kuomba radhi kwa mapungufu yoyote ambayo wageni wetu mtakuwa mmeyaona katika Wilaya yetu, Hili ni tukio la kwanza kabisa kubwa kufanyika hivyo ninaahidi kurekebisha dosari hizo katika matukio yajayo", Alimaliza Nkwega.
PICHA CHINI MKUU WA WILAYA YA MKALAMA MHESHIMIWA CHRISTOPHER NGUBIAGAI (ALIYEVAA KAUNDA SUTI KATIKATI) AKIKABIDHI ZAWADI YA BAISKELI KWA WANAFUNZI WA WILAYA HIYO WALIOFANYA VIZURI KATIKA MATOKEO YAO KUINGIA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2016.
No comments:
Post a Comment