Katika kuendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya
muungano wa Tanzaniai aliyoyatoa kwa viongozi wote wa uma wakati akiingia
madarakani, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mh. Christopher Ngubiagai (Aliyesimama)ametangaza
harambee inayotaraijiwa kufanyika Aprili 9,2016 kwa ajili ya kukusanya sehemu
ya fedha itakayotumika kutengeneza madawati 6295.
Ngubiagai amesema ameamua kuchukua hatua hiyo ili
kuhakikisha mpaka kufikia juni 30 mwaka huu hakuna mwanafunzi ambaye atakaa
chini hasa ukizingatia kuwa serikali imeamua kutoa elimu ya msingi na sekondari
bure hivyo ni lazima ihakikishe elimu hiyo inatolewa katika mazingira ya
kuridhisha.
“Awali madawati yaliyokuwa yakihitajika ni 6773 lakini
kuna wadau wametengeneza sehemu ya idadi hiyo na kubaki na idadi ya madawati
6295 ambayo gharama ya kuyatengeneza ni shilingi milioni 377 na laki 7 kwa
mchanganuo wa shilingi elfu 60 kila dawati” Amesema Ngubiagai.
Ametaja mikakati
ambayo yeye kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
pamoja na watumishi wengine waliamua kuichukua ili kufikia malengo ya kukusanya
kiasi hicho cha pesa au idadi hiyo ya madawati ambayo ni pamoja na Kufanya
harambee itakayowashirikisha wadau wa elimu, wazawa na wananchi wenye mapenzi na maendeleo ya
Wilaya ya Mkalama kwa ujumla.
Ameongeza lengo la harambe hiyo ni kukusanya kiasi cha
shilingi milioni 150 huku kiasi kingine
cha pesa kilichobaki kikitarajiwa kukusanywa
kupitia pesa ya mfuko wa mbunge, baadhi ya taasisi ikiwemo benki ya NMB
ambayo imeshakubali kuchangia sehemu ya madawati hayo, wananchi mbalimbali ambao
wamehamasishwa kupitia mikutano ya vijiji na wadau wa sekta ya elimu.
Aidha amepongeza hatua ya watumishi wa halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama kuahidi kuchangia sehemu ya idadi ya madawati hayo
yaliyobakia ambapo ametoa rai kwa wadau wa Elimu na wananchi mbalimbali
watakaoguswa na jambo hili kujitokeza kwa wingi siku ya harambee ili kuweza
kuhakikisha hakuna mwanafunzi wa Wilaya ya Mkalama anayekaa chini ifikapo juni
30 mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment