Siku mbili tu baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kutoa
agizo kwa watendaji kutekeleza kwa vitendo amri ya Rais wa Tanzania Mh. John
Pombe Magufuli ya Vijana kutocheza mchezo wa Pool muda wa asubuhi na kabla ya
saa 10 jioni, hatimaye serikali kupitia Mkurugenzi wa bodi ya michezo ya
kubahatisha, Abbas Tarimba (pichani juu) imetaja adhabu ya faini kwa wale watakaokiuka amri
hiyo.
Akizungumza mchana wa leo, Tarimba amesema kuwa wachezaji wa
mchezo huo hasa vijana sasa watalazimika kusubiri hadi saa 10 kamili jioni
ndipo wacheze mchezo huo au wakubali kulipa faini ya shilingi laki tatu (300,000) kama wakikiuka amri hiyo.
“Tumetayarisha barua ambazo zitatumwa kwa wakuu wa mikoa ili
kuelekeza wananchi kanuni, sheria na taratibu za mchezo huo”.
Amesema kuwa barua hizo pamoja na matangazo yatakayotoka
kwenye vyombo vya habari, yatatoa muongozo kwa wachezaji wa mchezo huo ambapo kwa
siku za kazi utaanza saa 10:00 jioni mpaka saa 5:00 usiku na siku za mapumziko
utaanza saa 8:00 mchana mpaka saa 6:00 usiku.
Tarimba amesema kuwa faini hiyo inatokana na sheria ya
michezo ya kubahatisha (Gaming Act) kifungu cha 52 katika kifungu kidogo cha
kwanza sura ya 42 inayosema asiye na kibali cha kuchezesha au atakayekiuka
kanuni za mchezo huo atashtakiwa na akikutwa na hatia atalazimika kulipa faini
ya shilingi 300000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote viwili.
|
No comments:
Post a Comment